Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 30, 2025 Local time: 11:30

Marekani yawataka waasi wa M23 kuacha kuelekea Goma


Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya nje ya Seneta Jim Risch, Mrepublikan-Idaho, akizungumza wakati wa kikao cha kamati, Oktoba 18, 2023, mjini Washington. (Picha ya AP)
Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya nje ya Seneta Jim Risch, Mrepublikan-Idaho, akizungumza wakati wa kikao cha kamati, Oktoba 18, 2023, mjini Washington. (Picha ya AP)

Wanajeshi wa DRC  walizuia jaribio la waasi wanaoungwa mkono na Rwanda usiku kucha katika mji wa Goma, mashariki mwa nchi hiyo vyanzo viwili vya jeshi la Congo vilisema Jumamosi, baada ya sauti za mashambulizi makubwa ya mabomu kuutikisa mji huo saa za alfajiri.

Hali ilionekana kuwa shwari katika mji mkuu wa jimbo hilo lenye zaidi ya watu milioni 1 kufikia Jumamosi asubuhi huku watu wakitoka nje kufanya biashara zao huku kukiwa na uwepo mkubwa wa polisi, waandishi wa habari wa Reuters walisema.

Uasi wa miaka mitatu wa M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yenye utajiri mkubwa wa madini umeongezeka mwezi Januari huku waasi wakichukua udhibiti wa maeneo mengi zaidi kuliko hapo awali na kuapa siku ya Ijumaa kuuteka mji wa Goma.

Vikosi vya Congo vilizuia mashambulizi katika mji huo usiku kucha kwa kuweka safu ya ulinzi, chanzo cha jeshi la Congo kilisema.

Pia wanajeshi watatu wa Afrika Kusini waliuwawa na takriban wengine 14 walijeruhiwa katika mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo siku ya Alhamisi, jeshi la Afrika Kusini lilisema katika taarifa yake Jumamosi.

Wakati huo huo mwenyekiti wa kamati ya uhusiano wa Kigeni, Seneta Jim Risch Mrepublikan kutoka Idaho ametoa taarifa akisema "waasi wa M23 lazima waache mara moja kusonga mbele kuelekea Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC, na kuongezea lazima pande zote zinazohasimiana kuacha uhasama, kurejesha upatikanaji usio na masharti wa misaada ya kibinadamu, na kuheshimu ahadi zao kwa mujibu wa mkataba wa Luanda.

Kushindwa kwa utawala wa Biden kuziwajibisha pande zinazohusika kwa ukiukaji wa siku za nyuma kumewatia nguvu wahusika wa mapigano ya duru hii ya sasa. Mzozo wa Mashariki mwa Congo umesababisha mamilioni ya watu kuhama makazi yao, na kusababisha ukatili mkubwa hasa dhidi ya wanawake na watoto na kuliyumbisha eneo muhimu usalama na uchumi wa kikanda na Marekani. Watu wa Congo wanastahili mazuri zaidi na pande zote za mzozo huu lazima zichukue hatua za haraka kukomesha mapigano haya”.

Nayo Serikali ya jimbo la Kivu Kaskazini,huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imesema kamwe haitasalimu amri kwa waasi wa M23 na kuwaonya kuwa jeshi la FARDC liko tayari kuulinda mji huo kwa hali yoyote ile.

Naibu Gavana wa jimbo hilo, Epuka Lipopo ameiambia Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika kuwa kamwe hawataruhusu mji mkuu huo kuangukia kwenye mikono ya waasi na wanajeshi wa serikali wako kati tahadhari kubwa ya kuulinda mji huo pamoja na raia wake.

Wakati hayo yakijiri inaelezwa kuwa gari la walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCO limeshambuliwa na waasi na inasadikiwa walinzi wawili wameuawa katika shambulizi hilo.

Forum

XS
SM
MD
LG