Rais wa Marekani Joe Biden amezungumzia vita vya Ukraine hii leo Alhamisi huko White House na kusema kuwa pia wataipa msaada wa silaha nzito. Msaada wa Marekani kwa Ukraine unajiri wakati rais wa Russia Vladimir Putin amewaamuru wanajeshi wake kutokivamia kiwanda cha chuma kilichoko katika mji wa Mariupol nchini Ukraine, ambako kuna wanajeshi wa Ukraine.
Putin amemwambia waziri wake wa ulinzi Sergei Shoigu, katika kikao kilichoonyeshwa kwenye televisheni kwamba wanajeshi wa Russia wanastahili kukizingira kiwanda hicho kiasi kwamba hata nzi asipate nafasi ya kupita, akiongezea kwamba hatua ya kukishambulia kiwanda hicho itawaweka wanajeshi wa Russia katika hatari isiyokuwa na maana yoyote. Shoigu amemwambia Putin kwamba wanajeshi 2,000 wa Ukraine wamo katika kiwanda cha Azovstal.