Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 09:49

Marekani yaishtumu Afrika Kusini kuipa silaha Russia katika vita vyake nchini Ukraine


Meli ya Russia, Lady R, ikitiwa nanga kwenye kituo cha majini cha Simon Town, karibu na mji wa Cape Town, Afrika Kusini, Disemba 8, 2022.
Meli ya Russia, Lady R, ikitiwa nanga kwenye kituo cha majini cha Simon Town, karibu na mji wa Cape Town, Afrika Kusini, Disemba 8, 2022.

Marekani Alhamisi imeishutumu Afrika Kusini kuipa silaha Russia katika vita vyake nchini Ukraine kwenye operesheni ya siri ya siku tatu ya majeshi ya majini karibu na mji wa Cape Town mapema mwezi Disemba mwaka jana.

Balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini Reuben Brigety amesema katika maoni yaliyotangazwa na vyombo kadhaa vya habari vya Afrika Kusini kwamba Marekani ina uhakika kwamba silaha hizo zilipakiwa kwenye meli ya mizigo yenye bendera ya Russia, Lady R, ambayo iliegeshwa kwa siri kwenye kituoa cha majini cha Simon Town kabla ya kuondoka na kuelekea Russia.

Alizitaja tuhuma za Afrika Kusini kuipa silaha Russia wakati wa uvamizi wake nchini Ukraine kuwa “zenye uzito mkubwa” na kusema anatilia shaka msimamo wa Afrika Kusini wa kutoegemea upande wowote katika mzozo wa Ukraine.

Bungeni, kiongozi wa chama cha siasa cha upinzani, John Steenhuisen alimuuliza Rais Cyril Ramaphosa ikiwa Afrika Kusini “inawapa silaha wanajeshi wa Russia ambao wanaua na kutesa watu wasio na hatia.”

Ramaphosa alijibu kwamba uchunguzi unafanyika. “Suala hili linachunguzwa, na wakati ukifika tutaweza kulizungumzia,” Ramaphosa alisema lakini alijizuia kutoa maelezo zaidi.

Baadaye katika taarifa, Ramaphosa alisema maafisa wa Marekani na Afrika Kusini walijadili kuhusu suala hilo la meli ya Lady R, na walikukabilana kwamba uchunguzi utaendelea, na kwamba idara za ujasuzi za Marekani zitatoa ushahidi wowote zilionao.

XS
SM
MD
LG