Serikali ya Marekani ina wasi wasi mkubwa na amri iliyotolewa na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza hapo Novemba 2 akilitaka jeshi la usalama la nchi hiyo kutumia nguvu kufanya upekuzi majumbani kusaka silaha na waasi katika muda wa siku tano.
Katika taarifa iliyotolewa na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power alisema Marekani imestushwa sana na kusambaa kwa ghasia nchini Burundi na matamshi ambayo yameonyesha wazi yanaweza kuchochea hali ya khofu na mivutano kote nchini.
Bibi Power alisema wamesikitishwa sana na ripoti ambazo ni za kichochezi na hotuba za kuwagawa watu zinatumiwa pia na maafisa wengine wa serikali.
Rais wa Baraza la Senate nchini Burundi, Reverien Ndikuriyo, aliripotiwa kutumia lugha za vitisho ambazo hazijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 20.
Balozi wa Marekani alisema iwe ni kwa lugha ya Kirundi au kiingereza matamshi ya lugha hiyo yana vitisho, “ unawaambia wale wanaotaka kutekeleza operesheni: katika suala hili, watumie nguvu zote, watu hawa wanafaa kufa. Nawaamuru, nendeni.”
Taarifa ya Bibi. Power iliongezea kuwa hotuba kama hizi ni hatari sana na kuitaka serikali ya Burundi kuwaruhusu haraka, bila ya masharti yoyote wafuatiliaji wa haki za binadamu na wa usalama wa Umoja wa Afrika kuingia nchini humo na haraka kuchukua hatua kwa ahadi yake ya kushiriki katika majadiliano ya kimataifa nje ya Burundi ili kufikia muafaka katika kurejesha uthabiti na kumaliza hali ya khofu nchini humo.