Marekani imesema inatafuta taarifa kuhusu Mohamoud Abdi Aden, ikimuelezea kuwa kiongozi wa kundi la Al-Shabaab lenye makao yake Somalia ambalo liliendesha mashambulizi kadhaa mabaya katika nchi jirani ya Kenya.
Kundi hilo mshirika wa Al-Qaeda lilikiri kuhusika katika uvamizi wa Januari 15, mwaka 2019 wa hoteli ya DusitD2 mjini Nairobi ambao ulidumu saa 20.
Watu 21 walipoteza maisha , akiwemo raia wa Marekani, na wengine wengi walijeruhiwa. Kenya ilisema wakati huo kwamba washambuliaji wote waliuawa.
“Mohamoud Abdi Aden, kiongozi wa Al-Shabaab, alikuwa katika mtandao uliopanga shambulio la hoteli ya DusitD2,” balozi wa Marekani nchini Kenya, Meg Whitman, aliwaambia waandishi wa habari mjini Nairobi.
Amesema Marekani inatoa zawadi ya hadi dola milioni 10 kwa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa Aden.