Leo imetimia miaka 10 tangu Septemba 11, 2001, yalipotokea mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Marekani na kuuwa karibu watu 3,000 na kuligeuza taifa la Marekani ambalo lilikuwa likidhani liko salama kutokana na mashambulizi katika ardhi yake.
Kutoka New York hadi Washington anga ilikuwa wazi na bluu asubuhi ile wakati ndege mbili za abiria zilizotekwa zilipogonga katika minara ya majengo ya World Trade Center mjini New York na nyingine kupiga katika makao makuu ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani - Pentagon.
Ndege ya nne iliyotekwa ilianguka karibu na mji mdogo wa Shanksville, Pennsylvania, baada ya abiria kupambana na watekaji na kuchukua udhibiti wa ndege hiyo.
Ilipofika mwishoni mwa 2001, Marekani ilikuwa katika vita na Afghanistan. Miaka miwili baadaye Marekani ilivamia Iraq. Wakati huo huo, taifa lilibadili idara zake za ulinzi wa ndani, na kuunda Wizara ya Ulinzi wa Ndani ya nchi, kubadili sheria ili kuzuia uwezekano wa mashambulizi mengine kama hayo kutokea.
Wakati Wamarekani wanakumbuka na kuadhimisha, Rais Barack Obama anatembelea maeneo yote ambayo mashambulizi yalitokea. Katika hotuba yake ya kila wiki alisifu wafanyakazi za uokozi waliojaribu kuokoa maisha wakati wa mashambulizi yale.
Mapema mwaka huu, vikosi maalum vya Marekani vilifanikiwa kumwua kiongozi wa al-Qaida Osama bin Laden huko Pakistan na kutimiza ahadi aliyoitoa rais wa zamani wa Marekani George W. Bush.