Wasiwasi kuhusu kile ambacho kinaonekana kama kutopunguzwa kwa vikwazo ilivyowekewa Iran pamoja na mazungumzo ya kisiasa yanayoelekea kusambaratika yanatarajiwa kuzungumziwa wakati wa mkutano kati ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Iran.
Kerry na Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Javad Zarif, watakutana leo New York, wakati Kerry akiwa anaanza ziara ambayo pia itampeleka hadi Misri na Saudi Arabia.
Maafisa wa Iran wamelalamika kwamba nchi yao haijapunguziwa vikwazo, kama ilivyokubaliawa katika azimio la kihistoria kuhusu program yake ya nyuklia ilililotiwa saini mwezi Januari.
Akiwahutubia waandishi wa habari huku akiandamana na mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, Zarif alisema ni sharti mataifa yote yachukue hatua zifaazo ili kuondoa vizingiti kwa utekelezaji wa makubaliano hayo .