Marekani inatathmini tena malalamiko yake kwa Nigeria ya hivi karibuni ya kusitisha kwa muda huduma ya Twitter hatua ambayo maafisa waandamizi wa Marekani walisema ni ishara ya kudhibiti nafasi ya kisiasa katika nchi hiyo kubwa sana huko Afrika magharibi.
Mamlaka ya Nigeria ilisitisha huduma ya Twitter mwanzoni mwa mwezi huu kwa muda usiojulikana baada ya kampuni ya mtandao wa kijamii yenye makao yake Marekani, ilipofuta "tweet" iliyotolewa na Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari kwa kukiuka kanuni za huduma.
Kusimamishwa kwa muda kwa Twitter kulileta wasiwasi na bado huduma hiyo inaendelea kuwa chanzo cha wasi wasi, alisema Akunna Cook, naibu waziri wa mambo ya nje kwa masuala ya Afrika, wakati wa mazungumzo yake ya Jumatatu kwa njia ya video yaliyoandaliwa na Atlantic Council yenye makao yake Washington.
Cook, binti wa wahamiaji wenye asili ya Nigeria alisema nchi hiyo inaweza kuchukua jukumu muhimu la kuijenga Afrika magharibi, lakini ishara za kufungwa nafasi za kisiasa, na ishara za kuzuia uhuru wa kuzungumza zinatisha.