Mivutano na ushindani baina ya Marekani, China, na Russia inaelezwa kuhatarisha juhudi za kukabiliana na janga la Covid-19.
Kuongezeka kwa mivutano ya mataifa hayo kulionekana wazi katika mikutano ya pembeni ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa, siku ya Alhamisi.
Inaelezwa hali hiyo inatishia kufunika juhudi za kimataifa za kukabiliana na maambukizo ya corona.
Baraza kuu la mwaka huu limefanyika kwa njia ya mtandao, kutokana na janga la corona, na limekuwa likiangazia zaidi namna ya kukabiliana na Covid-19.
Mikutano ya pembeni imefanyika katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ikiwa na jukumu la kushugulikia jambo hilo.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameonyesha kuwa na wasiwasi kwamba janga hili la corona linaimarika kutokana na uwepo wa mvutano wa siasa za kikanda.
Amesema kwamba janga hili ni jaribio kwa ushirikiano wa kimataifa, jaribio ambalo jumuiya ya kimataifa imeshindwa.