Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 14:30

Marais wa Kenya na Tanzania waahidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kibiashara


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, kulia akimsikiliza rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa mkutano wao na waandishi huko Ikulu ya Nairobi, May 4, 2021.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, kulia akimsikiliza rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa mkutano wao na waandishi huko Ikulu ya Nairobi, May 4, 2021.

Kenya na Tanzania zitaendelea kushirikiana kuwekeza katika nyanja mbalimbali za kiuchumi ili kuinua uwezo wa nchi hizo mbili za Afrika Mashariki. Haya yamesemwa na marais wa nchi hizo Rais Uhuru Kenyatta na mgeni wake Samia Suluhu Hassan.

Ziara ya siku mbili ya Rais Samia Suluhu jijini Nairobi miaka mitano baada ya mtangulizi wake, hayati John Pombe Magufuli kufika Nairobi, inapokelewa na mwamko mpya na raia wa Kenya ambao wanahisi ni ishara nzuri ya kuwepo mahusiano bora ya kibiashara, kiuchumi na kidiplomasia kati ya mataifa haya mawili, wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Afrika Mashariki.

Mara tu baada ya mazungumzo ya faragha ya pande mbili kati ya serikali za nchi mbili, Rais Samia Suluhu na mwenyeji wake Uhuru Kenyatta, wamewaeleza wanahabari kuwa Nairobi na Dodoma zitaendelea kudumisha na kuboresha mahusiano ya muda mrefu ili kuwawezesha raia wake kunawiri katika sekta mbalimbali kama vile biashara, uwekezaji, utalii, utamaduni, michezo na harakati za kutokomeza ugaidi.

Marais hao wametia saini mikataba mbalimbali ikiwemo; mkataba wa kujenga bomba la gesi kutoka Dar es salaam hadi Mombasa ili kuongeza usambazaji wa umeme na gesi katika mataifa hayo mawili. Kenya na Tanzania, zimeeleza kuwa zinafufua usafiri wa Ziwa Victoria kutoka Jinja Uganda, Kupitia Kisumu Kenya, Mwanza hadi Bukoba nchini Tanzania.

Aidha, Rais Samia na mwenyeji wake Uhuru Kenyatta wamekubaliana kuimarisha tume ya ushirikiano wa pande mbili kuondoa vikwazo visivyokuwa vya ushuru ili kurahihisha uendeshaji wa biashara kati raia wa nchi hizi jirani.

Rais Kenyatta ametumia nafasi hii kumshukuru mno Rais Samia kwa kuitikia mwito wake wa kuzuru Nairobi baada ya kumtumia mjumbe maalum Waziri Amina Mohamed Aprili 10 katika ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na kumwahidi kuwa Kenya itaendelea kuwa mshirika wake wa karibu.

Rais Kenyatta amemhakikishia mgeni wake kuwa serikali yake itaendelea kufanya biashara na Tanzania, kuimarisha mihimili iliyowekwa na marais waliotangulia, kuondoa vikwazo vyovyote vilivyopo, viwe vya kibiashara au kidiplomasia.

Awali kulikuwa na vuta nkuvute kati ya Kenya na Tanzania mara kwa mara, na sintofahamu iliyotokana na mvutano huo, ilisababisha kudorora kwa mahusiano haya. Mvutano wa hivi karibuni, ni kuhusu katazo la Kenya kuingiza mahindi kutoka Tanzania kwa madai ya Kenya kuwa yalikuwa na sumu kuvu.

Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan anaeleza kuwa huu ni muamko mpya kwa nchi hizi mbili.

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa pana haja ya Kenya na Tanzania kushirikiana kubuni mpango mkakati wa kupunguza maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha kuwekwa kwa vikwazo vya kibiashara.

Ziara hii inajiri chini ya mwezi mmoja baada ya Rais Samia kufanya ziara ya kiserikali nchini Uganda ambako pamoja na Rais Yoweri Kaguta Museveni, waliweka makubaliano ya pande tatu kukamilisha mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Rais Kenyatta, anaeleza kuwa akiwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pana haja ya kuongeza ufanyikaji wa biashara wa ndani kwa ndani katika jumuiya hii.

Akiwa Nairobi, Rais Samia anatarajiwa kuhutubia mkutano unaowaleta pamoja wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania Jumatano, nia ikiwa ni kujadili mambo yanayodumisha biashara na uwekezaji katika mataifa haya mawili.

Pia, Jumatano mchana, atahutubia kikao cha pamoja cha bunge la Kenya—yaani baraza la Senate na bunge la Taifa—miaka saba baada ya rais wa Tanzania wakati huo Jakaya Mrisho Kikwete kufaya hivyo.

Lakini kabla kuondoka Nairobi, Rais Samia ametoa mwaliko kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Nairobi.

XS
SM
MD
LG