Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 20:17

Mapigano Sudan: Hakuna ishara ya mazungumzo, wafungwa wameachiliwa huru kwa kukosa chakula


Moshi kutoka kwa vitu vinavyochomeka wakati jeshi la serikali likipambana na wapiganaji wa RSF katika mji wa Khartoum, Sudan, April 15, 2023. PICHA: Reuters
Moshi kutoka kwa vitu vinavyochomeka wakati jeshi la serikali likipambana na wapiganaji wa RSF katika mji wa Khartoum, Sudan, April 15, 2023. PICHA: Reuters

Mapigano yameripotiwa Sudan, saa chache baada ya kutangazwa muda wa kusitisha mapigano hayo huku kukiwa hakuna ishara ya pande zinazopigana kufanya mazungumzo.

Jeshi la Sudan (SAF) na kundi la wapiganaji la (RSF) walikuwa wamekubaliana kusitisha mapigano kwa muda was aa 72 kuanzia Jumanne, baada ya kufanyika mazungumzo yaliyoongozwa na Marekani na Saudi Arabia.

Lakini milio ya risasi imesikika Jumanne jioni katika eneo la Omdurman, mojawapo ya miji ya Khartoum karibu na mto Nile ambapo jeshi la Sudan limetumia ndege zisizokuwa na rubani kulenga sehemu zinazoshikiliwa na RSF.

Jeshi la Sudan vile vile limetumia ndege zisizokuwa na rubani kuwasukuma nyuma wapiganaji wa RSF kutoka sehemu kulipo kiwanda cha kusafisha mafuta katika mji wa Bahri, ambao ni wa tatu kw ukubwa katika Blue Nil na White Nile.

Mjumbe maalum wa umoja wa mataifa kwa ajili ya Sudan Volker Perthes, ameambia baraza la usalama la umoja wa mataifa jumanne kwamba kuna ishara kwamba makubaliano ya kusitisha vita yanatekelezwa.

Hakuna ishara za mazungumzo

Volker Parthes hata hivyo amesema kwamba “hakuna upande umeonyesha nia ya kutaka kufanya mazungumzo, na kwamba kila upande una Imani ya kushinda vita hivyo.”

“Haya ni maamuzi yasiyo sahihi,” amesema Parthes, akiongezea kwamba uwanja wa ndege wa Khartoum unafanya kazi lakini barabara ya ndege imeharibiwa.

Tangu vita kati ya jeshi la Sudan na kundi la RSF vilipoanza April 15, na kusitisha mpango wa kuirejesha nchi hiyo chini ya utawala wa kidemokrasia, mapigano yamekuwa yakiendelea katika sehemu zinazokaliwa na watu, ambapo jeshi la serikali limekuwa likiwalenga wapiganaji wa RSF kwa kutumia mashambulizi ya angani.

Watu 459 wameuawa na zaidi ya 4000 kujeruhiwa. Hospitali zimeharibiwa huku kukiwepo uhaba wa chakula katika nchi hiyo ambayo theluthi tatu ya watu milioni 46 wanategemea msaada wa chakula.

Wafungwa wanaotafutwa na mahakama ya ICC wameachiliwa huru

Katika kile kinachoonekana kama kuharibika zaidi kwa hali ya usalama, aliyekuwa waziri katika serikali ya Sudan, Ahmed Haroun, anayetafutwa na mahakama ya uhalifu ya kimataifa ICC kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika eneo la Dafur, amesema kwamba ameachiliwa huru pamoja na wenzake, kutoka gereza la Kober.

Haroun amesema kwamba hali katika gereza la Kober imekuwa mbaya sana katika siku za hivi karibuni.

Mtu aliyekamatwa kwa kufanya maandamano na kuzuiliwa katika gereza hilo, amesema kwamba wafungwa wameachiliwa huru baada ya kukosekana maji na chakula kwa muda wa wiki nzima.

Haroun amesema kwamba watu wengine ambao wameachiliwa huru ni pamoja na waliokuwa maafisa katika serikali ya aliyekuwa rais Omar al-Bashir aliyeingia madarakani kupitia mapinduzi ya mwaka 1989 na serikali yake kuanguka mwaka 2019 kufuatia maandamano ya raia.

Mahakama ya ICC inamtafuta Haroun kwa kupanga mashambulizi ya dhidi ya raia katika eneo la Dafur kati ya mwaka 2003 na 2004. Haijabainika kuhusu mahali alipo Omar al-Bashir.

Mkuu wa jeshi la Sudan Lt. Gen. Abdel Fattah al-Burhan (kushoto) na kamanda wa kundi la RSF Mohamed Hamdan Daglo (kulia)
Mkuu wa jeshi la Sudan Lt. Gen. Abdel Fattah al-Burhan (kushoto) na kamanda wa kundi la RSF Mohamed Hamdan Daglo (kulia)

Mabalozi, wafanyakazi wa kutoa msaada na raia wa kigeni wanaendelea kuondoka Sudan

Nchi kadhaa zimeendelea kuwaondoa raia wake kutoka Sudan.

Pamoja na wanaoondoka ni mabalozi na wafanyakazi wa kutoa msaada.

Kuna wasiwasi kwamba huenda mapigano yakawa mabaya zaidi iwapo makubaliano ya kusitisha vita kwa muda wa siku tatu yatamalizika.

Timu ya usalama wa kitaifa, ya utawala wa rais wa Marekani Joe Biden, inaendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa kijeshi katika pande mbili zinazopigana ili kuacha mapigano na kutoa msaada wa kibinadamu.

Mapigano yamekwamisha shughuli katika hospitali na huduma zingine muhimu, huku watu wakiwa wamekwama nyumbani kwao.

Shirika la kutoa msaada wa kimatibabu la Medecins Sans Frontieres (MSF) limeripoti kwamba miili ya watu imetapakaa barabarani.

Shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi limesema kwamba huenda maelfu ya watu kutoka Sudan wakakimbilia katika nchi Jirani.

XS
SM
MD
LG