Mapigano makali kati ya vikosi vya serikali inayotambuliwa kimataifa ya Yemen na waasi wa ki-Houthi yameibuka tena Jumapili na kuongeza wiki ya ghasia katika mkoa wa kimkakati wa Marib, nchini Yemen, maafisa wamesema. Huku darzeni ya watu wakiwa wameuwawa, mapigano haya yanatia shaka kubwa juu ya juhudi zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa za kuanzisha tena mazungumzo ya kumaliza miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Waasi wanaoungwa mkono na Iran, mapema mwezi huu walifanya tena shambulizi kwenye jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta, ngome inayopinga wa-Houthi inayoshikiliwa na serikali inayotambuliwa kimataifa. Lakini walikabiliwa na upinzani mkali na hawajaweza kusonga mbele kufuatia idadi kubwa ya vifo kutoka kwa wa-Houthi, maafisa wa jeshi kutoka pande zote mbili wamesema.
Vita vya Yemen vilianza mwaka 2014, wakati waasi walipokamata mji mkuu, Sanaa, na sehemu kubwa ya kaskazini mwa nchi hiyo. Ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia na kuungwa mkono na Marekani uliingilia kati miezi kadhaa baadae kuwaondoa wa-Houthi na kuirejesha serikali inayotambuliwa kimataifa. Mzozo huo umeuwa takribani watu 130,000 na kusababisha maafa mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.
Waasi wanataka kupata udhibiti wa Marib, kufunga mpaka wa kusini wa Saudi Arabia na kuchukua udhibiti wa kisima cha mafuta katika jimbo hilo ambalo litawapa faida katika mazungumzo ya Amani.
Wakishtushwa na msukumo mpya wa wa-Houthi, ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia ulifanya mashambulizi ya mabomu kusonga mbele katika jangwa karibu na Marib. Pia ilileta majeshi ya nchi kavu kutoka mikoa inayoshikiliwa na serikali ya Taiz na Shabwa, viongozi hao walisema.
Ofisi ya vyombo vya habari vya wa-Houthi imeripoti Jumanne kwamba angalau mashambulizi ya anga 10 yalifanywa na ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia huko Marib, na mashambulizi ya anga zaidi ya mawili yamefanywa kwenye jimbo jirani la Jaw, ambalo waasi hutumia kama kituo cha kufanya mashambulizi yao ya hivi karibuni huko Marib.
Zaidi ya wapiganaji 48 waliuwawa na zaidi ya 120 walijeruhiwa katika siku mbili zilizopita, wengi wao wakiwa wa-Houthi, maafisa hao wamesema. Zaidi ya darzeni mbili nyingine wameripotiwa kuuwawa mwanzoni mwa shambulizi ambalo limejikita zaidi katika wilaya za Sarouh na Makhdara, wameongeza.
Maafisa hao wamezungumza kwa sharti ya kutotajwa majina kwa sababu hawakuruhusiwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.