Serikali ya Kinshasa, siku ya Alhamisi imewatuhumu wapiganaji wa kundi la M23 - wanaopambana nao mashariki mwa nchi kwa zaidi ya mwezi mmoja - kwa mauaji ya watu 50 katika kijiji cha Kishishe karibu kilomita 70 kaskazini mwa mji wa Goma.
M23 imejibu mara moja ikidai kwamba tuhuma hizo 'hazina msingi" wowote na kukanusha kwamba inawalenga raia.
Msemaji wa serikali Patrick Muyaya amesema kwamba wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri siku ya Ijumaa Rais Felix Tshisekedi, "amelaani vikali mauaji ya zaidi ya wananchi 100 huko Kishishe."
Amesema Tshisekedi "ameitaka serikali kutangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa," akiongezea kwamba bendera zitapepea nusu mlingoti kote nchini wakati huu.
"Kipindi cha maombolezo kitamalizika Jumatatu kwa kufanyika tukio la kuchangisha fedha ili kusaidia waathirika wa mauaji hayo," alisema Muyaya.
Tangu ripoti za mauaji hayo ya halaiki kutokea, kumekuwepo na wito wa kufanyika uchunguizi huru umezidi kujitokeza.
Muyaya anasema kwamba Rais "amemtaka waziri wa sheria kufanya uchunguzi mara moja na wakati huo huo kupanga uchunguzi wa kimataifa ufanyike ili kumulika uhalifu huu wa vita. ."