Wanafamilia walikuwa na simanzi walipopita kwenye jeneza lenye mwili wa Lemekani Nyirenda, mwenye umri wa miaka 23 katika Kanisa la Baptist la Lusaka, ambalo alikuwa muumini kabla ya kuhamia Russia.
Nyirenda aliandikishwa na kundi la mamluki la Russia, Wagner mwaka jana alipokuwa akitumikia kifungo cha miaka tisa na nusu kwa kosa la kutumia dawa za kulevya na kupelekwa kupigana Ukraine.
Kifo chake mwezi Septemba kilizua mzozo wa kidiplomasia, huku Zambia ikitaka maelezo ya haraka kutoka Kremlin.
Tanzania, Jumanne ilithibitisha mwanafunzi mwingine, Nemes Tarimo, aliuawa baada ya kuandikishwa gerezani na kundi la Wagner.
Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Stergomeba Tax alisema, Tarimo alipewa fursa ya kujiunga na kundi la Wagner kwa malipo na ahadi kwamba angeachiliwa baada ya vita vya Ukraine, ambapo Tarimo alikubali, na akapelekwa Ukraine ambako aliuawa Oktoba 24.
Katika miezi ya hivi karibuni, wanaume wameandikishwa kutoka magereza ya Russia kupigana kwenye mstari wa mbele nchini Ukraine kwa ahadi ya kupunguziwa adhabu na fedha za kuvutia.
Tarimo, alikuwa akisoma Russia toka 2020, alikamatwa Machi 2022 na kuhukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi.