Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 14:06

Mambo 15 muhimu unayostahili kufahamu kuhusu uchaguzi wa Kenya 2022


Kenya : Picha ya bendera ya Kenya
Kenya : Picha ya bendera ya Kenya

Kenya inajiandaa kwa uchaguzi wa 7 tangu nchi hiyo tajiri zaidi Afrika mshariki kuanza mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, miaka 30 iliyopita. Uchaguzi wa mwaka huu 2022 ni wa tatu tangu kupatikana kwa katiba 'mpya' mwaka 2010. Yafuatayo ni mambo muhimu 15 ambayo ni muhimu kujua

1

Agosti 9 2022 ndio tarehe ya upigaji kura. Kulingana na katiba ya Kenya, uchaguzi mkuu lazima uandaliwe Jumanne ya pili ya mwezi Agosti ya mwaka wa tano baada ya uchaguzi wa awali. Huu ndio uchaguzi wa tatu kuandaliwa baada ya kupitishwa kwa katiba ya mwaka 2010

2.

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ndio yenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi mkuu na kutangaza washindi. Tume hiyo ina makamishna 7.

3.

Kuna wagombea 4 wa urais; Dr. William Ruto ambaye ni naibu rais wa sasa, aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, wakili George Luchiri Wajackoya na wakili ambaye pia ni mhubiri kanisani David Mwaure Waihiga. Kati ya wagombea wenza 4, watatu ni wanawake, nao ni Martha karua, Justina Wamae na Ruth Wambui Mucheru. Rigathi Gachagua ni mgombea mwenza wa William Ruto. Gachagua ni mwanamme.

4.

Ushindani mkubwa ni kati ya naibu wa rais Dr. William Ruto (55) na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga (77). Ruto na Odinga waliwahi kuwa katika chama kimoja cha KANU wakati wa utawala wa aliyekuwa hayati rais Daniel Arap Moi, na pia ni ndio waanzilishi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

5.

Ruto anagombea urais kwa mara ya kwanza. Hii ni mara ya 5 kwa Raila. Alishindwa mara 4 za awali. Raila amekuwa akikataa kukubali matokeo katika mara nne ambazo amegombea urais na kupoteza.

6.

Jumla ya wapiga kura 22,120,458 wamesajiliwa kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu. Idadi ya juu zaidi ya wapiga kura (172,088) wamesajiliwa katika eneo bunge la Ruiru. Eneo bunge la Lafey lina idadi ndogo zaidi ya wapiga kura (18,564) Wafungwa 7,863 watashiriki katika upigaji kura. Wanawapigia wagombea wa urais pekee. Raia wa Kenya 10,443 wanaoishi ughaibuni walisajiliwa kypiga kura na watatekeleza zoezi hilo kwenye ubalozi wa Kenya kwenye nchi wanayoishi.

7.

Qatar inaongoza kwa idadi kubwa ya wakenya wanaoishi nje ya nchi hiyo watakaoshiriki katika zoezi la kupiga kura (1,437). Nchi nyingine ni Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Afrika Kusini, Ujerumani, Uingereza, Umoja wa Falme za Kiarabu, Canada na Marekani.

8.

Vijana wenye umri wa miaka 35 wanachangia asilimia 39.84 pekee ya idadi ya jumla ya wapiga kura. Nusu ya wapiga kura ni wanaume (50.88%). Wanawake ni asilimia 49.12. Lamu ndio Kaunti yenye idadi ndogo ya wapiga kura (81453). Nairobi inaongoza kwa idadi ya wapiga kura (2,415,310) kati ya kaunti zote 47.

9.

Kuna nafasi 1,882 za kujaza. Kuna wagombea 16,098. Nafasi 1 ya rais, 47 za magavana, 47 maseneta, 47 wawakilishi wa wanawake kutoka kila kaunti, wabunge 290 na wabunge wa kaunti 1,450. Kanuti ya Tana River inaongoza kwa kuwa na wagombea wengi wa ugavana (13), huku Narok ikiwa na idadi ya chini ya wagombea wa ugavana(2). Kwa jumla, wagombea 266 wanatafuta kuwa magavana katika kaunti 47 kote Kenya. Jumla ya wagombea 341 wanawania useneta katika bunge la senate lenye nafasi 47. Maeneo bunge ya Mvita, Gatundu Kaskazini, Kajiado Kaskazini na Mugirango Kaskazini ndiye yenye idadi kubwa ya wagombea wa ubunge (16 kila eneo bunge). Kuna nafasi za bunge 290 kote Kenya.

10.

Chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Dr. William Ruto, tayari kina mwakilishi wa akina mama (Beatrice Kemei, kaunti ya Kericho), ambaye ameidhinishwa na IEBC kuwa mwakilishi wa wanawake baada ya kukosa mshindani. Kuna wagombea 359 wa nafasi ya kuwakilisha wanawake katika kaunti 46 zilizosalia.

11.

Tume ya uchaguzi IEBC itatumia daftari mbili za wapiga kura – la karatasi na la digitali – daftari la karatasi litatumika iwapo mashine zitafeli kumtambua mpiga kura.

12.

Mshindi wa kura za urais ni lazima apate zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa. Ni lazima pia apate asilimia 25 ya kura zilizopigwa katika kaunti 24.

13.

Tume ya uchaguzi ina muda wa hadi siku 7 (wiki moja) kutoka siku ya kupiga kura, kutangaza mshindi wa kura za urais. Jaji mkuu na rais anayeondoka madarakani ni lazima wafahamishwe kwa maandishi kuhusu matokeo hayo. Endapo mshindi hapatikani katika duru ya kwanza ya uchaguzi, duru ya pili itaandaliwa kati ya wagombea waliomaliza katika nafasi ya kwanza na ya pili, ndani ya muda wa siku 30.

14.

Mtu yeyote ambaye hajaridhika na matokeo ya uchaguzi wa urais, ana haki ya kuwasilisha kesi katika mahakama ya juu ndani ya siku 7 baada ya matokeo rasmi kutangazwa. Mahakama ina muda wa siku 14 kufanya uamuzi wake. Uchaguzi unarudiwa ndani ya muda wa siku 60 endapo mahakama inafutilia mbali matokeo yaliyotangazwa.

15.

Mhula wa rais Uhuru Kenyatta utamalizika pale rais mpya atakapoapishwa.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG