Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 14:51

Makundi ya waasi DRC kukabiliwa na jeshi la Afrika mashariki


Wanajeshi wa DRC wakijadiliana namna ya kupambana na waasi wa M23 katika mlima wa Kibumba, kilomita 5 kutoka mji wa Goma.
Picha kutoka Maktaba. AP
Wanajeshi wa DRC wakijadiliana namna ya kupambana na waasi wa M23 katika mlima wa Kibumba, kilomita 5 kutoka mji wa Goma. Picha kutoka Maktaba. AP

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana Nairobi Kenya na kujadiliana kuhusu vita vinavyoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hii ni baada ya kundi la waasi la M23 kudhibiti mji wa Bunagana. Sehemu hiyo pia imeshuhudia ongezeko la ujumbe wa chuki katika jamii. Mkutano wa viongozi hao ni wa tatu kujadili hali ya usalama DRC.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haitaki wanajeshi wa Rwanda kushirikishwa katika jeshi la pamoja kwa ajili ya kupambana na waasi mashariki mwa DRC.

DRC imesema kwamba inakubali pendekezo la rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, kutuma jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini humo, kupambana na waasi wa M23, lakini haiwezi kuruhusu wanajeshi wa Rwanda kuwa sehemu ya mpango huo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kenyatta, alitangaza wiki iliyopita kwamba jeshi la jumuiya hiyo linastahili kuingia DRC mara moja na kupambana na makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo. Kenyatta alisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya kushauriana na marais wenzake wa Jumuiya ya Afrika mashariki.

Taarifa ya ikulu ya Nairobi ilisema kwamba jeshi hilo litashika doria katika sehemu za Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini na kulisaidia jeshi la DRC kwa ushirikiano na jeshi la Umoja wa zmataifa MONUSCO.

Sehemu jeshi la Afrika mashariki litashika doria

Kenyatta alitaka sehemu za Ituri, Kivu Kaskazini ikiwemo Bunagana, Bugusa, sehemu za Petit Nor, Masisi, Lubero, Beni-kasindi, na sehemuza Kivu Kusini kutangazwa kuwa sehemu ambazo silaha haziruhusiwi bila idhini ya serikali na kwamba makundi yote yanayobeba silaha yapokonywe silaha hizo kwa lazima.

Makamanda wa jeshi kutoka majeshi ya nchi zinazoshiriki, walikutana Nairobi Jumapili Juni 19 kuweka mikakati ya kuingia DRC.

Nabende wa Moto ni mchambuzi wa siasa na usalama wa Maziwa Makuu. Mfanyakazi mstaafu katika wizara ya ulinzi, Uganda. Yupo kampala, Uganda.

“Hilo linaweza kufanikiwa tu iwapo amri zitakuwa zinatoka kwa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na wala sio kwa makamanda wa kila nchi. Awepo kamanda mmoja anayeteuliwa na uongozi wa jumuiya nzima. Viongozi wamechoma kusuluhisha swala la DRC kisiasa na sasa ni nguvu za vita zitumike.” Amesema Nabende.

Zaidi ya makundi ya waasi 100 yanapigana DRC

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ina zaidi ya makundi ya waasi 100.

Kundi la waasi la CODECO pekee ndilo limekubali kuacha vita. Makundi ya waasi yametekeleza mauaji na kulazimuisha mamilioni ya watu kutoroka makwao mashariki mwa DRC. Kando na hayo, yamesababisha mvutano mkubwa wa kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na jirani yake ambaye ni Rwanda. Mgogoro huo vile unatishia amani na usalama wa jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki na kanda ya Maziwa mMkuu.

Kumekuwepo taarifa za vyombo vya habari kwamba jeshi la Rwanda limekuwa katika maandalizi ya kulinda mpaka wake kutokana na vita vya DRC.

DRC inaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23. Rwanda inaishutumu DRC kwa kuunga mkono waasi wa FDLR katika sehemu ya Kivu Kaskazini. FDLR ni kundi linaloshutumiwa na Rwanda kwa kusababisha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Rwanda inadai kwamba waasi wa FDLR wamekita mizizi katika jeshi la DRC na hata wana vyeo vikubwa katika jeshi hilo.

“Rwanda ina wasiwasi. Congo iliwaalika wanajeshi wa Uganda kupambana na waasi wa ADF. Wanajeshi hao wanaongozwa na generali Muhanga Kayanja. Wasiwasi wa Rwanda ni kwamba nchi zinaungana kijeshi na kuiacha nje. Wakati huo, Rwanda haikuwa na uhusiano mzuri na Uganda, Burundi sawa na ilivyo na DRC. Mpaka wa Uganda na Rwanda kufunguliwa haikuwa kwa sababu ya Muhoozi Kainerugaba, ni kwa sababu Kagame alijua hatari iliyokuwepo ya kutengwa na watu anaowaona kama maadui.” Amesema Nabende wamoto.

DRC haitaki jeshi la Rwanda kuhusishwa katika oparesheni maalum

Hatua ya DRC kutaka Rwanda isishiriki katika jeshi la pamoja la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki, inajiri baada ya waasi wa M23, ambao DRC imedai kila mara kwamba wanaungwa na Rwanda, wamedhibithi mji wa Bunagana baada ya mapigano makali na jeshi la DRC.

Mapigano hayo yalipelekea wanajeshi wa DRC kukimbilia Uganda, hatua ambayo imeonekana kama kudalilisha pakubwa jeshi la DRC, na ambayo inaripotiwa kumkasirisha sana rais wa DRC Felix Tshisekedi.

Msemaji wa jeshi laUganda UPDF Brigedia general Felix Kulaigye, aliambia kipindi cha kwa undani cha Sauti ya Amerika VOA wiki iliyopita kwamba wanajeshi 137 wa DRC walikuwa wamekimbilia Uganda na kujisalimisha katika kambi ya Kisoro. Wanajeshi kadhaa walikuwa wanatibiwa majeraha ya risasi katika hospitali tofauti kusini magharibi mwa Kisoro na Kabale, nchini Uganda.

DRC imesitisha mikataba yake na Rwanda

DRC imesitisha baadhi ya mikataba ya ushirikiano na Rwanda. Safari za ndege za Rwanda kwenda DRC zimepigwa marufuku. Mikataba ya uchimbaji wa madini nayo imepigwa marufuku.

Kamanda wa jeshi la ardhi la Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba, aliandika ujumbe wa twiter wiki iliyopita kwamba alikuwa ameamurishwa na babake yake, ambaye ni rais Yoweri Museveni, kusitisha oparesheni ya kijeshi dhidi ya kundi la Allied democratic forces ADF, kwa sababu ambazo hakufafanua.

Lakini jeshi la Uganda lilitoa taarifa kufutilia mbali taarifa hiyo na kusema kwamba oparesheni hiyo itaendelea. Jeshi la DRC vile vile lilitoa taarifa kufutilia mbali taarifa ya Muhoozi. Wachambuzi wanasema kwamba huenda hii ilitokana na wakuu wa usalama kutaka Uganda nayo kutoshirikishwa na maswala ya usalama wa DRC.

“Vitu vyovyote vinavyohusu jeshi. Sio jeshi la Uganda tu bali kila jeshi duniani, haviandikwi kwa mitandao ya kijamii kiholela. Jemedari Muhoozi anapenda sana kuandika maswala ya jeshi kwa mitandao ya kijamii. Hiyo ni hatari kwa kamanda wa jeshi. Alipotangaza kwamba jeshi la Uganda litaondoka Congo, hapo ikabidi serikali ijibu kwa haraka na hata rais akajitokeza na kusema oparesheni ya Congo inaendelea. Hiyo ni sintofahamu.” Amesema Nabende wamoto, mchambuzi wa siasa za maziwa makuu.

Ripoti ya utafiti kuhusu Uganda, ADF, Rwanda na M23

Ripoti ambayo imetolewa na kundi la Congo la utafiti CRG katika chuo kikuu cha New York kwa ushirikiano na Ebuteli, ambayo ni taasisi ya utafiti nchini DRC, imesema kwamba operesheni ya Uganda dhidi ya waasi wa Allied Democratic Forces – ADF, mashariki mwa DRC, ambayo ilianzishwa kwa ushirikiano kati ya DRC na Uganda, ilikuwa na lengo kubwa la kulinda machimbo ya mafuta ya Uganda katika ziwa Albert, mpakani na DRC.

Ripoti hiyo inasema kwamba oparesheni hiyo iliikasirisha Rwanda na kuwa sehemu ya kuanza mapigano makali ya kundi la M23 ambao DRC inasisitiza kwamba wanaungwa mkono na Rwanda. Akiwa Congo Brazaville, rais wa DRC Felix Tshisekedi alisema kwamba hana shaka yoyote kwa waasi wa M23 wanaungwa mkono na Rwanda.

Wanajeshi wa Uganda na wa DRC wamesema kwamba oparesheni dhidi ya waasi wa ADF imefanikiwa, lakini ripoti hiyo inasema kwamba operesheni imefanikiwa tu kuwasukuma waasi wa ADF kutoka karibu na mpaka wa Uganda lakini wamejikusanya katika makundi manne ndani ya DRC, na haijamaliza nguvu za ADF wenye uwezo wa kujiksanya kwa haraka bila kukata tamaa.

Waandishi wa ripoti wanasema kwamba kujihusisha kwa Uganda katika vita vya ADF nchini DRC, kuliikasirisha sana Rwanda. Uganda vile vile inajenga barabara ndani ya Congo. Uhusiano kati ya Uganda na Rwanda umekuwa mbaya katika siku za hivi karibuni, lakini umeanza kuimarika baada ya mtoto wa rais wa Uganda Muhoozi Kainerugaba kuanza mazungumzo na rais wa Rwanda Paul Kagame.

‘Yeye ametangaza kwamba ana uhusiano wa ndani sana na jemedari Paul Kagame wa Rwanda. Kiusalama, congo inaweza kuwa na wasiwasi na kujiuliza hatua inazochukua. Jemedari Muhoozi ni rafiki ya Jemedari Kagame, Jemedari Muhoozi anaongoza oparesheni ya jeshi la Uganda Congo. Je, itakuwa salama tukiruhusu Uganda katika jeshi la pamoja? Congo lazima ijiulize hilo. Bunge la Congo limejadili swala hilo wakati wakizungumzia kukosa Imani na Rwanda. Kuna wabunge walitaja Uganda.” Amesema Nabende.

Rwanda imekana madai ya kusaidia waasi wa M23

Maelfu ya raia wa DRC wamekimbilia Uganda kama wakimbizi.

Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Biruta alisema hivi karibuni kwamba wapiganaji wa M23 ni raia wa DRC wenye hasira yao, wasiofurahishwa na uongozi wa sasa wa nchi yao. Alisisitiza kwamba hilo ni swala la ndani ya Congo.

Biruta alisema kwamba waasi wa M23 ambao walikimbilia Rwanda mwaka 2013 walipokonywa silaha na wanaendelea na mapigano yao mbali na mpaka wa Rwanda. Alisema kwamba Rwanda ilisimamia mchakato wa kuwarudisha DRC waasi wa M23 waliokuwa wamekimbilia Rwanda lakini serikali ya DRC imekataa kuheshimu makubaliano.

Rwanda inaishutumu DRC kwa kuendelea kufyatua makombora ndani ya Rwanda, akisema kwamba Rwanda haitanedelea kuvumilia uchokozi huo.

“Haya mashambulizi yakiendelea, Rwanda itakuwa na haki ya kuyajibu kwa ajili ya kulinda usalama wa watu wake. Tuna uwezo wa kufanya hivyo.” Alisema Biruta katika kikao na waandishi wa habri siku chache zilizopita mjini Kigali.

DRC inataka jumuiya ya kimataifa kuishinkiza Rwanda kuacha ‘kuunga mkono M23’

Rwanda inapoandaa mkutano wa jumuiya ya madola (CHOGM) wiki hii mjini Kigali, rais wa DRC Felix Tshisekedi ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono DRC na kumshindkiza rais wa Rwanda Paul Kagame kumaliza vita dhidi ya Congo na kuamurisha wanajeshi wake, ambao anadai wameingia DRC, kusababisha vifo na uhalifu wa kivita dhidi ya watu wa DRC.

Tshisekedi amesisitiza kwamba DRC ina haki ya kutaka jirani wake waheshimu mpaka wa DRC. Amesema kwamba watu wa DRC wanataka Amani na wanatafuta usalama wa taifa lao. Ametaka washirika wa DRC wa kimataifa, Afrika, Marekani na hasa Uingereza kuishinkiza Rwanda kuacha kuunga mkono waasi wa M23, madai ambayo amesisitiza kila mara. Amesisitiza Uingereza kwa kuzingatia makubaliano ya hivi karibuni kati ya Uingereza na Rwanda ya kiasi cha dola milioni 150 kuwapeleka Rwanda wahamiaji wanaoingia Uingereza kinyume cha sheria ina uwezo wa kuishinkiza Rwanda.

Alipotembelea DRC, mfalme wa ubelgiji Philipe, alikutana na waakilishi wa asasi za kiraia june 9 na kusisitiza kwamba swala la mpaka wa DRC kuheshimiwa ni muhimu sana kwa Ubelgiji, ambayo ilikuwa mkoloni wa DRC. Philipe aliahidi kusaidia DRC kwa kila hali kushinda nguvu waasi wa M23.

“Congo ina raslimali nyingi ambazo kila mtu anataka. Viongozi wa wanachama wa Jumuiya ya Madola wanaweza kuzungumzia swala hilo la Amani nchini Congo, lakini kuhusu madai ya Rwanda kuunga waasi wa M23, wataomba ushahidi wa kutosha kutoka kwa DRC.” Amesema Nabende Wamoto.

Shinkizo zaidi la kutaka vita kumalizika

Umoja wa Afrika umeitaka DRC kufanya mazungumzo na Rwanda kumaliza mgogoro huo. Wachambuzi wanasema mgogoro huu unatishia umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambao DRC ni mwanachama mpya.

Katika mahojiano na sauti ya Amerika wiki iliyopita, mchambuzi wa maswala ya Usala Richard Tuta akiwa Nairobi, aliambia sauti ya Amerika kipindi cha kwa undani, kwamba jeshi la pamoja la Afrika mashariki ni hatua nzuri lakini itakabiliwa na vizingii kadhaa ikiwemo vya kisheria na ufadhili wake.

Mkutano wa mwezi April, wa viongozi wa Kenya, Uganda, Burundi, DR Congo na Rwanda, ulikubaliana kuunda jeshi la pamoja kusaidia Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Imetyarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG