Rais Joe Biden, akitangaza makubaliano hayo Jumatano siku chache kabla ya kuondoka madarakani, amemtaka mrithi wake kutekeleza makubaliano hayo muhimu ambayo yanafungua njia ya ujenzi wa Gaza iliyoharibiwa na vita.
“Hatimaye, naweza kutangaza makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka yamefikiwa kati ya Israel na Hamas,” Biden alisema katika hotuba huko White House.
Aliongeza “Mapigano huko Gaza yatasitishwa, na karibuni mateka watarejea katika familia zao.”
Afisa mkuu wa utawala wa Biden aliwambia waandishi wa habari kwamba wawili kati ya mateka raia wa Marekani ambao wako hai, Keith Siegel na Segui Dekel Chen, watakuwa miongoni mwa mateka wa kwanza watakaoachiliwa. Afisa huyo alizungumza na waandishi wa habari kwa masharti ya kutotajwa jina.
Makubaliano hayo yataanza kutekelezwa Jumapili, siku ya mwisho kwa Biden kuwa madarakani.
Maafisa wa Gaza wanasema zaidi ya raia 46,000, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, waliuawa katika operesheni za jeshi la Israel huko Gaza.
Forum