Taarifa za jeshi la Kenya zinasema wanajeshi wake walishambuliwa na wapiganaji 45 wa al-Shabab Alhamis huku majeshi hayo yakisogea karibu na mji wa Al- Qoqani kusini mwa Somalia kudhibiti maeneo yake.
Taarifa hiyo inasema wapiganaji 9 wa al-Shabab wameuawa na wanajeshi wawili wa Kenya kujeruhiwa mmoja wao akiwa katika hali mahtuti. Wanajeshi hao inaripotiwa wamerudishwa Kenya kwa ndege kupata matibabu.
Akizungumza na Sauti ya Amerika msemaji wa jeshi la Kenya Meja Emmanuel Chirchir amesema “mapema asubuhi ya leo tumeweza kutumia ndege zetu kupiga ngome za al-Shabab katika mahala inayoitwa Anole na tukaweza kuvunja kambi yao ya mafunzo na kambi yao ya logistic”.
Wanajeshi wa Kenya wamechukua pia udhibiti wa mji wa Busar wakisogea kuelekea miji mingine miwili ya Burahache na Burgayo. Wanamgambo wa al-Shabab hawajatoa tamko hadi sasa juu ya mapigano ya leo.
Meja Chirchir, anasema mvua kali zinazuia kidogo kampeni yao lakini mambo yanaendelea vyeme na wameweza kusababisha hasara kidogo kwa al-Shabab maeneo ya kusini jambo ambalo wamekuwa wakidhumania kufanya ili kudhibiti maeneo hayo kabla ya wanaharakati kurudi na kuyateka tena kama walivyofanya wakati wa mashambnulizi ya Ethopia.