Chama cha MDC, kinadai kwamba tume ya uchaguzi ilifanya udanganyifu katika kuhesabu kura kitendo kilicho mnufaisha Rais Mnangagwa wa chama kinachotawala ( ZANU-PF).
Mnangagwa alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo uliofanyika Julai 30 baada ya kupata asilimia 51 ya kura zilizopigwa na kumshinda mpinzani wake Nelson Chamisa wa MDC, aliyepata asilimia 44.3.
Chamisa na chama chake cha MDC, kilipinga matokeo ya uchaguzi huo.
Chamisa amesisitiza kuwa chama cha MDC kina ushahidi wa kutosha kwamba tume ya uchaguzi kwa ushirikiano na chama kinacho tawala cha ZANU-PF, kilifanya udanganyifu katika kuhesabu kura na kwamba ana imani mahakama ya kikatiba itafutilia mbali matokeo hayo na kuamrisha uchaguzi kufanyika upya.
Uchaguzi wa Julai 30, ulikuwa wa kwanza kutomshirikisha kiongozi wa muda mrefu wa nchi ya Zimbabwe, Robert Mugabe, aliyeondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi.