Akizungmza Jumapili wakati akimuapisha Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Mwigulu Nchemba huko Chato Mkoa wa Geita, Rais Magufuli ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia watumishi wote wa umma wakiwemo walimu ambao ndio wengi zaidi kuwa serikali itaendelea kuwalipa mshahara hadi shule zitakapofunguliwa.
Amesema kuwa kuna nchi nyingine zimeshindwa kulipa mishahara watumishi wake, lakini Tanzania itaendelea kulipa.
“Tusihusishe hili la Corona kwenye uchumi wa nchi yetu, mimi nimepata uzoefu katika miezi miwili au mitatu tangu ugonjwa huu uingie. Nchi yetu asilimia 49 ya watumishi ni walimu ambao ndio wengi zaidi kuliko wengine," amesema Magufuli akiongeza kusema,
“Lakini tumeendelea kulipa mishahara bila hata wao kufundisha, kuna nchi zimeshindwa kulipa mishahara." Kiongozi huyo wa Tanzania alisisitiza kwamba "Nataka kuwathibitisha walimu tutaendelea kulipa mishahara yenu hadi shule zitakapofunguliwa, pia watumishi wengine wote tutaendelea kuwalipa mishahara na hii ndio dhana ya kutokuumiza uchumi kwa tatizo hili ambalo litaondoka.”
Akizungmza akiwa huko Chato, Rais Magufuli amefafanua hatua kwa hatua namna ambavyo serikali imeendelea kushughulikia janga la Corona na hali ilivyo.
Hata hivyo, amesema uzoefu unaonyesha kila linapotokea gonjwa jipya watu hupata hofu na wasiwasi. Ametoa mfano wakati Ukimwi unaingia nchini kupitia Mkoa wa Kagera kwa mara ya kwanza watu waliogopa sana, hata waliokuwa hawana Ukimwi nao walipakaziwa kuwa na Ukimwi.
“Leo hii ukizungumza kuna mtu ana Ukimwi bado watu wengine wanakwenda kuposa na kuoa na maisha yanaendelea kwasababu hofu yaugonjwa huo imeondoka," ameema Magufuli.
Kwa hiyo kwenye magonjwa watu wa umri wangu wanakumbuka, siku za nyuma wakati ugonjwa wa surua umeingia “Ilikuwa ukisikia kuna familia kuna surua hata kwenda kusalimia unaogopa kwamba mtaambukizwa surua lakini leo ni ugonjwa wa kawaida na hofu imeondoka,”amesema Rais Magufuli.
Amefafanua hali hiyo hiyo ilikuwa kwa magonjwa mengine ambayo yamekuwa yakitokea nchini. Magonjwa kama TB, magonjwa kama Ukoma yalikuwa yanatisha na kutia hofu.”Ukimuona mtu mwenye ukoma unajiuliza kuhusu maisha yake yatakuaje lakini sasa hakuna tena hofu kwenye magonjwa hayo.”
Pia amesema yametokea magonjwa megi kama Zika na Ebola katika nchi nyingine mbalimbali na hofu zilijengeka .”Niwaombe Watanzania tuondoe hofu na kubwa zaidi tuendelee kuchukua tahadhari.