Malaria ni ugonjwa ambao unaenezwa na mbu aliyeathirika, takriban nusu ya idadi ya watu duniani wako hatarini kuambukizwa Malaria. Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO, linakusudia kuutokomeza ugonjwa huo kufikia mwaka 2030.
Katika taarifa za afya zilizotolewa Januari mwaka huu huko Kenya ilielezwa kwamba dawa ya invo-mectrim ilitumika kama majaribio ya kuzuia Malaria nchini Kenya .
Ugonjwa wa Malaria ni changamoto kutokana na hali ya joto na mabadiliko ya hali ya hewa ingawa hali ni hivyo, mikakati inayotekelezwa na serikali na mashirika yasiyo ya serikali yamesaidia kupunguza mzigo wa ugonjwa wa Malaria kwa asilimia 50.
Usambazaji wa vyandarua kila baada ya miaka mitatu katika maeneo yaliyo na viwango vya juu vya mambukizo ya Malaria umesaidia kupunguza idadi ya maambukizi.
Tayari serikali kupitia mpango wa ufadhili wa rais wa Marekani umegawa vyandarua milioni 15 katika majimbo 22 kati ya 47 Kenya.
Wakati huohuo madaktari na watafiti nchini Kenya wamepongeza mpango wa WHO kupitisha chanjo ya Malaria katika mataifa matatu ya Afrika ikiwemo Kenya.
Baadhi ya mataifa ya Afrika ikiwemo Uganda na DRC yameathiriwa na ugonjwa wa Mpox uliozuka katikati ya mwaka huu. Agosti 26 mwaka 2024 WHO ilitangaza kwenye tovuti yake na kutoa taadhari kwa watu kujikinga na ugonjwa huo. Ilieleza dalili za ugonjwa zinaanzia siku moja hadi 21 baada ya kuambukizwa.
Mtu anayeambukizwa anapatwa na vipelele vinavyowasha kuliko kawaida, homa, koo kuvimba na kuwasha, maumivu ya kichwa na viungo vya mwili pamoja na kukosa nguvu mwilini.
Hata hivyo WHO iliandika kuwa kugundua ugonjwa wa Mpox unaweza kuwa changamoto kwa sababu maambukizo na hali vinaweza kufanana, hivyo kuwataka watu kuwa makini kutambua na kutofautisha kuhusu Mpox na Ndui (Chikcen Pox).
Miezi minne tu baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza dharura ya ulimenguni kutokana na ugonjwa wa Mpox - ambayo imeelemea mifumo ya afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwaka huu - ugonjwa mpya unaofanana na mafua ambao umeua makumi ya watu umezua hofu miongoni mwa watu wengi nchini DRC.
Kati ya Oktoba 24 na Desemba 11 mwaka huu, kulikuwa na zaidi ya visa 510 vya ugonjwa huo ambao haujatambuliwa vilivyoripotiwa katika maeneo manane kati ya 30 ya afya katika eneo la Panzi, kulingana na takwimu kutoka kwa mamlaka za afya za mitaa.
Wiki iliyopita Shirika la Afya Duniani WHO, ambalo limetuma wataalam katika eneo hilo kuchunguza chanzo cha mlipuko huo na kusaidia kukabiliana na ugonjwa huo, lilisema zaidi ya watu 30 walikufa hospitalini kutokana na ugonjwa huo.
Kulikuwa na vifo vingine zaidi ya 45 vilivyorekodiwa katika jamii za mbali huko Panzi, kwa mujibu wa Waziri wa Afya wa DRC, Roger Kamba.
Dunia iliadhimisha siku ya ukimwi duniani Desemba mosi ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa “ Hatua za Pamoja: Dumisha na kuharakisha maendeleo ya VVU”
Siku hii ilikuwa kwa ajili ya kuchochea uelewa, na kuwakumbuka wale walioathiriwa na VVU na Ukimwi , na kuweka nia ya dhati kutokomeza janga la Ukimwi.
Siku hii pia ni kwa ajili ya kuwaelimisha watu kupima afya zao kuangalia maambukizo ya ugonjwa huo na kuchukua hatua.
Hali ya usonji inakumbukwa April 2 kila mwaka kimataifa kwa ajili ya kuhakikisha watu wanafahamu vya kutosha kuhusu hali hii ambayo inawakumba zaidi watoto wadogo.
Siku hii ilipitishwa na baraza kuu la Umoja wa Mataifa Novemba mosi mwaka 2007 baada ya kupendekezwa na Moza Bint Nasser Al Missned , mwakilishi wa Umoja wa Mataifa huko Qatar na kuungwa mkono na wajumbe .
Forum