Maelfu ya raia wa Ethiopia waliandamana mjini Addis Ababa siku ya Jumapili kuunga mkono serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed huku wanajeshi wa serikali kuu wakipambana na waasi wanaotishia kuingia mjini humo.
Baadhi ya waandamanaji waliikashifu Marekani, ambayo ni miongoni mwa mataifa ya kigeni yenye nguvu ambayo yametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kwa vita vya mwaka mzima ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu huku kukiwa na ongezeko la mapambano ya waasi mwishoni mwa juma lililopita.
Marekani, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, na Kenya na Uganda zimetoa wito katika siku za hivi karibuni kusitishwa kwa mapigano.
Serikali ya Abiy imeahidi kuendelea kupigana. Siku ya Ijumaa, serikali ilisema ina jukumu la kulinda nchi yake , na kuwataka washirika wake wa kimataifa kusimama na demokrasia ya Ethiopia.
Baadhi ya waliokusanyika katika uwanja wa Meskel katikati mwa Addis Ababa walijifunika bendera ya taifa. Wengi waliishutumu Marekani kwa ukosoaji.
Utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden siku ya Jumanne uliishutumu Ethiopia kwa "ukiukaji mkubwa" wa haki za binadamu na kusema kuwa unapanga kuiondoa nchi hiyo kutoka kwenye makubaliano ya biashara ya Sheria ya Ukuaji na Fursa ya Afrika (AGOA).