Maelfu ya watu kutoka New York mpaka California Alhamisi walijazana kwenye mitaa ya miji mikubwa ya Marekani kwa siku ya tatu mfululizo kuonyesha kutoridhishwa na ushindi wa Donald Trump kuwa Rais wa 45 wa Marekani.
Maandamano yalishuhudiwa kuanzia Portland, Oregon hadi Chicago mpaka New York pamoja na miji mingine ingawa walioshiriki walikuwa wachache kuliko iliovyokuwa muda mfupi baada ya kudhihirika kuwa Trump angeshinda kwenye uchaguzi huo.
Alhamisi usiku, Trump alituma ujumbe kupitia ukurasa wake wa twitter akisema kuwa baada ya kushinda kwenye uchaguzi huo, sasa waandamanaji wamejitokeza baada ya kuchochewa na vyombo vya habari na hii si haki hata kidogo.
Mjini Portland Oregon, alhamisi usiku maelfu ya waandamanaji walizua fujo huku wakivunja vioo vya maduka na kuwasha moto barabarani kwa mujibu wa idara ya polisi mjini humo. Maafisa kutoka idara ya uchukuzi walilazimika kufunga kwa muda barabara kuu ya 25 karibu na mji wa Denver usiku wa kumkia Ijumaa.