Jeshi, ambalo limekuwa likizuia maandamano kama hayo katika siku za nyuma mjini Harare, Jumamosi lilionekana kuunga mkono waandamanaji hao, na kuwaelekeza kwenye uwanja ambako hotuba zilitolewa na wanaharakati, wanasiasa na wapiganiaji wa zamani wa ukombozi, waliomtaka rais huyo kujiuzulu.
Maandamano pia yalifanyika katika miji mingine nchini humo, wengi wakitoa wito huo huo, kwamba kiongozi huyo mkongweaondoke madarakani.
Mugabe alijitokeza hadharani kwa mara ya kwanza siku ya Ijumaa, tangu kuzuiliwa nyumbani kwake na jeshi siku ya Jumatano.
Jeshi lilichukua udhibiti wa vyombo vya dola, na kuongoza mazungumzo yaliyonuiwa kumshinikiza kiongozi huyo kuachia madaraka.
Wakati huo huo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson Ijumaa alitoa wito wa kufuatwa kwa katiba katika uongozi wa Zimbabwe na kusema kuwa ni haki ya raia wa nchi hiyo kuwa na serikali waitakayo kwa kufanya uchaguzi wa kidemokrasia na unaoheshimu haki binadamu.
Tillerson aliyasema hayo mjini Washingnton alipowahutubia mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za bara la Afrika.