Hatua hiyo inapeleka ujumbe mzito Korea Kaskazini ambayo wiki hii ilifanya jaribio la kombora la masafa ya kati hali ikikaidi azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linalokataza kurusha makombora hayo.
Kikundi cha Carl Vinson cha mashambulizi cha majeshi ya Marekani kilikuwa kimeweka nanga katika bandari ya Singapore na kinatarajiwa kuelekea Australia wakati Kikosi cha Pacific cha jeshi hilo kimeamrisha manuari hizo kuelekea Kaskazini badala yake.
“Manuari hizo za Third Fleet zinaelekea huko kwa shughuli maalumu: kuimarisha ulinzi wa eneo lenye maslahi ya Marekani Magharibi ya Pasifiki,” Kamanda Dave Benham, mkurugenzi wa operesheni za habari cha kikosi cha Pacific Command Third Fleet ameiambia VOA.
“Hatari namba moja katika eneo hilo inaendelea kutokana na Korea Kaskazini, kwa sababu ya kukosa umakini, kutosimamia majukumu yake, na programu yake ya kujaribu makombora na kuendeleza uwezo wake wa kufikia silaha za nyuklia kunakoleta matatizo.
Katika Kikundi hicho cha mashambulizi wenzake ni manuari inayobeba ndege za kivita, manuari nyingine USS Carl Vinson, na manuari tatu zenye nguvu za kuangamiza makombora.
Korea Kaskazini yakaidi
Pyongyang imeendelea kukaidi onyo la kimataifa juu ya kujaribu kwake makombora na vifaa vingine vya nyuklia.
Jumapili, afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini amekaririwa akisema katika vyombo vya habari vya serikali,akiahidi kuimarisha ulinzi wa nchi hiyo ilikujilinda na kitendo chochote cha mashambulizi ya makombora kama yale yaliyopigwa na Marekani nchini Syria wiki iliopita.
Afisa huyo ambaye hakutambuliwa kwa jina ameliambia Shirika la Kuu la Habari Korea mashambulizi hayo ya anga“hayawezi kamwe kusamehewa,” na inaonyesha kwanini Pyongyang inahaki ya kuwa na silaha za Nyuklia.
Mwaka huu maafisa wa Korea Kaskazini, ikiwa pamoja na kiongozi Kim Jong Un, wamerejea kusema kuwa majaribio ya kombora la masafa marefu linalofika kati ya mabara duniani au linalofanana na hilo inawezekana liko njiani, inawezekana mpaka ifikapo Aprili 15, ambayo ni sikukuu ya 105 tangu kuzaliwa kwa muasisi wa taifa la Korea Kaskazini na inayoazimishwa kila mwaka ijulikanalo kama “siku ya Jua.”
Wakati Rais Donald Trump hakueleza mkakati uliowazi wa namna ya kukabiliana na taifa hilo lililotengwa, amekosoa sera ya Marekani iliotumiwa na uongozi uliopita ya “mkatati wa kusubiri,” katika kukabiliana na Korea Kaskazini yenye kuendelea na juhudi zake za kutengeneza uwezo wa kupiga makombora ya nyuklia ya masafa marefu.
Trump ameitaka pia China, moja ya nchi chache ambazo zinamafungamano na Pyongyang, kuchukua hatua kuzuia utashi wao wa kuwa na silaha za nyuklia.
Mapema mwezi huu, Trump amesema kuwa huenda Marekani ikachukua hatua peke yake kama China haiko tayari kufanya juhudi zaidi kuidhibiti Korea Kaskazini.
“Kama China haijatatua tatizo la Korea Kaskazini, sisi tutachukua hatua,” Trump ameliambia Jarida la The Financial Times la April 2.
“China ni kati ya mawili watatusaidia na suala la Korea Kaskazini au hawatotusaidia. Wakitusaidia, hilo litakuwa jambo zuri kutoka kwa nchi China, na kama hawajafanya hivyo, na iwapo hawatafanya hivyo, halitokuwa jambo zuri kwa yoyote.”
Marekani, China zakubaliana
Imeripotiwa kuwa Trump amezungumzia suala la Korea Kaskazini na Rais wa China Xi Jinping wakati walipokutana wiki hii huko Florida.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson amesema kuwa viongozi hao wawili wamekubaliana kwamba suala la utengenezaji wa silaha unaofanywa na Pyongyang umefikia hatua ya hatari, lakini hapakuwa na maelezo zaidi juu ya hatua gani ingechukuliwa na nchi hizi mbili ilikuzuia programu hiyo ya silaha ya Pyongyang.
Wasaidizi wa Trump katika usalama wa taifa wamemaliza kupitia maamuzi mbalimbali yakuweza kuidhibiti Korea Kaskazini katika programu yake ya nyuklia na makombora. Maamuzi haya ni pamoja na hatua za vikwazo vya uchumi na kijeshi lakini vitaegemea sana upande wa vikwazo na shinikizo juu ya Beijing kumdhibiti jirani yake wa karibu.
Hata hivyo chaguo la kutumia nguvu za mashambulizi ya kijeshi kuizuia Korea Kaskazini kuendeleza juhudi zake za silaha za nyuklia bado lipo palepale, japokuwa katika kuliangalia suala hilo inaonekana kipaumbele kipo katika hatua zenye kuzuia madhara na kutosisitizwa kwa hatua za kijeshi.