Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:13

Maadhimisho ya siku ya kumaliza utumwa Marekani yavutia kampeni za uchaguzi


Rais Joe Biden akisaini amri ya kiutendaji ya kuadhimisha siku ya kumaliza mfumo wa kutumia watumwa, Juneteenth National Independence Day ACT, June 17, 2021.
Rais Joe Biden akisaini amri ya kiutendaji ya kuadhimisha siku ya kumaliza mfumo wa kutumia watumwa, Juneteenth National Independence Day ACT, June 17, 2021.

Maadhimisho ya siku ya kutangaza kumalizika kwa mfumo wa kutumia watumwa Marekani, maarufu Juneteenth yanaonekena kuvutia kampeni za kisiasa kuelekea uchaguzi wa mwezi Novemba.

Wagombea wawili wakuu, Rais Joe Biden na Donald Trump, kila mmoja anatafuta uungwaji mkono kutoka kwa Wamarekani weusi, ambao ndio waliathirika zaidi wakati wa enzi ya utumwa.

Rais Joe Bien alianda mapema sherehe za Juneteenth kwa tamasha maalum katika white House.

“Historia yetu sio kuhusu yaliyopita pekee yake, inahusu yanayotokea leo na siku za baadae. Suala ni ikiwa mustakbali huo wetu utakuwa kwa sisi sote au kwa baadhi yetu tu,” alisema.

Biden amesema wapinzani wake wa kisiasa wanajaribu kuandika upya historia.

“Hao ni wazimwi wa kale waliovaa nguo mpya wanaojaribu kuturudisha nyuma, kutupokonya uhuru wetu, kuifanya kuwa vigumu kwa watu weusi kupiga kura au kura yako kuhesabiwa. Kufunga milango ya nafasi zote. Kushambulia thamini ya mchanganyiko wetu, usawa na kuhusisha kila mtu.”

Kampeni ya Donald Trump ilizindua muungano wa Wamarekani weusi kwa ajili ya Trump siku ya Jumamosi, huku rais wa zamani akijaribu kuwavutia wapiga kura weusi katika kanisa moja mjini Michigan.

“Ni sehemu muhimu ya jamii yetu. Tumewafanyia mengi na nina sema hili, na ninasema kwa kujivunia kwamba nimefanya mengi kwa ajili ya jamii ya watu weusi kuliko rais yeyote tangu Abraham Lincoln. Hii ni kauli muhimu,” Trump alisema.

Alisema wapiga kura weusi wanapoteza ajira zao kwa kile alichokitaja kuwa ni kwa sababu ya wahamiaji haramu.

“Kila jimbo ni jimbo la mpakani. Umesikia jambo hilo. Basi wanakuja katika miji yenu na kuchukua kazi zenu. Wanawaathiri zaidi Wamarekani wenye asili ya ki Afrika na baada ya hapo wenye asili ya Amerika Kusini kuliko jamii nyingine yeyote ile.”

Trump anasema jamii ya watu weusi wanaumia zaidi kutokana na uhalifu chini ya utawala wa Biden.

“Uhalifu umeongezeka zaidi hivi sasa na katika miji ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika, na watu wengi wanaokutana namii wanasema , mheshimiwa tunataka ulinzi. Tunataka polisi kutulinda. Hatutaki kuibiwa, hatutaki kushambuliwa na kupigwa au kuuliwa kwa sababu eti tu tunataka kuvuka barabara kwenda kununua mkate.”

Takwimu za idara ya upelelezi wa jinai FBI zinaonyesha uhalifu wa kutumia nguvu Marekani umepungua sana kote nchini katika miji mikubwa na midogo.

Biden anasema wapiga kura weusi walimwezesha kupata ushindi miaka minne iliyopita na anahitaji msaada wao tena

“Kwa sababu ya kura ya Wamarekani weusi, Kamala na mimi ni rais na makamu rais wa Marekani kwa sababu yenu. Kwa sababu ya kura zenu , Donald Trump alishindwa. Na kwa kura yenu mwaka 2024 tutamfanya Donald Trump kushindwa tena,” alisema.

Miaka minne iliyopita ni asilimia 8 tu ya watu weusi waliompigia kura Trump . Utafiti wa maoni ya wananchi wa kituo cha Pew wakati wa kampeni ya mwaka huu unaonyesha asilimia18 ya watu weusi wanamuunga mkono Trump, ongezeko kubwa ambalo linaweza kuleta mabadiliko katika ushindani ulio wa karibu sana, hasa katika majimbo yenye ushindani mkali kama Michigan.

Forum

XS
SM
MD
LG