Mkutano huo utasusiwa na ma rais wa Guatemala, Honduras na Mexico na wengine kama njia ya kupinga uamuzi wa Washington wa kuzitenga kwenye mkutano huo serikali za Cuba, Nicaragua na Venezuela.
Kutokuwepo ma rais sita tayari imeleta dosari kwenye mkutano wa kilele unaoangaliwa kama fursa kubwa ya kushughulikia changamoto zinazolikabili eneo hilo, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa usalama wa kiuchumi, afueni baada ya janga la covid, mabadiliko ya hali ya hewa, uhamiaji na mgawanyiko wa kisiasa.
Ukikabiliwa na shinikizo la kisiasa ndani ya nchi, ikiwemo lile la jamii zilizo uhamishoni katika jimbo la Florida, utawala wa Biden uliamua kwamba Cuba, Nicaragua na Venezuela hazikidhi vigezo vya mkataba wa 2011 wa kidemokrasia kati ya nchi za Amerika ambao unasisitiza demokrasia kama jambo la msingi.
Washington ilitangaza rasmi kwamba nchi hizo zimeondolewa kwenye orodha ya washiriki, tarehe 5 Juni, siku moja kabla ya hafla hiyo kuzinduliwa.