Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 19:48

M23 wametakiwa kuweka silaha chini kufikia Ijumaa saa kumi na mbili jioni


Meja Jenerali Jeff Nyagah (katikati) kamanda wa kikosi cha jeshi la jumuiya ya Afrika mashariki nchini DRC Nov. 16, 2022.
Meja Jenerali Jeff Nyagah (katikati) kamanda wa kikosi cha jeshi la jumuiya ya Afrika mashariki nchini DRC Nov. 16, 2022.

Makundi yote ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, yameamurishwa kuweka chini silaha ifikapo Ijumaa wiki hii, saa kumi na mbili jioni la sivyo wakabiliwe na jeshi la jumuiya ya Afrika mashariki.

Uamuzi huo umetangazwa baada ya kikao kilichoongozwa na rais wa Angola Joao Lourenco na kuhudhuriwa na rais wa DRC Felix Tshisekedi, Evariste Ndayishimiye wa Burundi na mjumbe wa amani wa jumuiya ya Afrika mashariki Uhuru Kenyatta.

Mkutano wa viongozi hao umetoa amri ya kusitishwa mapigano ifikapo Ijumaa Novemba 25 na makundi yote ya silaha hasa la M23 wanaodai kwamba wanapigania haki za watu kutoka kabila la Watutsi mashariki mwa DRC, kuondoka katika miji ambayo linashikilia ikiwemo mji wa Bunagana.

Waasi watapewa ulinzi na jeshi la DRC, jeshi la jumuiya ya Afrika mashariki na wanajeshi wa umoja wa mataifa Monusco endapo watajisalimisha.

Wanajeshi wa Kenya na Burundi tayari wapo DRC na Uganda inatarajiwa kutuma wanajeshi 1000 wiki ijayo.

Rwanda imewakilishwa na waziri wa mambo ya nje

Maamuzi ya Luanda yamejiri siku chache baada ya aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kusema kwamba rais wa Rwanda Paul Kagame, anayetuhumiwa kuunga mkono waasi wa M23, ameahidi kushawishi waasi hao kuacha vita. Rwanda imewakilishwa kwenye mkutano wa Jumatano na waziri wa mambo ya nje Vincet Biruta.

Kundi la M23 limekuwa likisisitiza kwamba kamwe halitaacha vita. Nabende Wamoto, mchambuzi wa siasa za maziwa makuu anasema kwamba waasi hawawezi kushinda jeshi la jumuiya endapo kuna ukweli na nia njema kutoka kwa nchi wanachama.

“Wakati waasi wa M23 waliposikia kwamba wanajeshi wa Kenya wanaenda DRC, kiliimarisha mapigano ili kiweze kudhibithi sehemu kubwa ya DRC ndipo kionekane kama ni kikundi kikubwa kinachistahili kusikilizwa na wala sio kushambuliwa kwa mabomu. Huu ulikuwa ni ujumbe wa kisiasa. Lakini iwapo viongozi wa jumuiya wanaiungana kwa ukweli, kahuna kikundi kitasalia DRC maana makundi yote ya waasi nchini humo yanaungwa kisiasa,” amesema Nabende.

DRC inashutumu inashutumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23 huku Rwanda ikishutumu DRC kwa kuunga mkono waasi wa FDLR. Mkutano wa Luanda, pia umekubaliana kuacha kabisa ushirikiano wowote wa kisiasa na kundi la M23 na makundi yote ya waasi nchini DRC.

Mtoto msichana akiwa ameshika mkono wa mpiganaji wa kundi la waasi la M23. Karuba, Goma. Nov 28,2012
Mtoto msichana akiwa ameshika mkono wa mpiganaji wa kundi la waasi la M23. Karuba, Goma. Nov 28,2012

Mchakato wa kisiasa kati ya makundi ya waasi na serikali

Mkutano pia unataka kuwepo mpango wa kuwarudisha nyumbani wakimbizi wa DRC, kuazishwa mchakato wa kisiasa kati ya serikali ya DRC na makundi ya waasi na kurejea uhusiano mwema kati ya DRC na Rwanda.

Jean Mulumba, kiongozi wa kundi la wazalendo, linalodai kusaidia serikali kupambana na makundi mengine ya waasi, hata hivyo anasema hawawezi kuwacha chini silaha na hawataheshimu makubaliano ya Angola.

“Rwanda na Uganda zinastahili kuacha kuingiza silaha nchini mwetu, zinazotumika kuua watu wetu, kubaka mama na wasichana wet una kupora mali yetu. Wanataka kuimarisha sera zao za utawala katika nchi za maziwa makuu. Kama hawataacha kuleta nchini metu silaha, hatutawacha kupigana.”

Usafirishaji wa mizigo kutoka Kenya na Uganda kuelekea DRC umekwama

Mapigano ya waasi mashariki mwa DRC yameathiri biashara na kusababisaha hasara kubwa, mizigo kutoka Kenya na Uganda ikikosa kuingia DRC, Kando na Bunagana, waasi wa M23 wanashikilia mji wa Rutshuru na kufunga mpaka kati ya Ishasha na Kanungu na hivyo kufunga kabisa mipaka yote kati ya Uganda na DRC.

Waasi hao pia wanashikilia mipaka ya Kitigoma na Busaza na magari ya mizigo kutoka Kenya na Uganda yamekwama katika mpaka wa Ishasha.

Waasi wa Allied democratic forces ADF, nao wameendelea kutekeleza mashambulizi na kuua raia mashariki mwa Congo, mashambulizi ya Jumatano yakisababisha vifo vya watu 16.

XS
SM
MD
LG