Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 03:26

M23 wamedhibithi sehemu zaidi ya 14, Kagame na Tshisekedi wamekubali kupunguza uhasama


Wapiganaji wa kundi la M23 wakitembea katika mji wa Karuba, kilomita 62 magharibi mwa Goma, Kivu kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokasia ya Congo. PICHA: Reuters
Wapiganaji wa kundi la M23 wakitembea katika mji wa Karuba, kilomita 62 magharibi mwa Goma, Kivu kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokasia ya Congo. PICHA: Reuters

Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame wamekubaliana kupunguza uhasama na hali ya wasiwasi ambayo imekumba nchi hizo kutokana na mashambulizi ya kundi la waasi la M23 mashariki mwa DRC.

Viongozi hao wamekubaliana hayo katika mkutano uliofanyika mjini Luanda, Angola Jumatano.

Mgogoro wa kidiplomasia umekuwa ukiongezeka kwa kasi sana kati ya majirani hao wawili, tangu kundi la waasi la M23 lilipoanza mashambulizi mashariki mwa Congo mwishoni mwa mwezi March.

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imedai kwamba Rwanda inaunga mkono waasi wa M23, lakini Kigali imekanusha madai hayo na badala yake kushutumu Congo kwa kuunga mkono waasi wa FDLR wenye lengo la kuangusha utawala wa rais Paul Kagame.

Congo na Angola zimetoa taarifa, Rwanda imesalia Kimya

Mkutano wa Angola umesimamiwa na rais Joao Lourenco ambaye ni mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika kutatua mgogoro huo.

Taarifa ya serikli ya Congo uliochapishwa na ofisi ya rais Tshisekedi kwenye ukurasa wake wa Twiter baada ya kikao cha Luanda umesema kwamba “mkutano kati ya Rwanda, DRC na Angola umekubaliana kupunguza uhasama kati ya Rwanda na Congo.”

Viongozi hao wamekubaliana kwamba “mapigano yakome mara moja na waasi wa M23 waondoke nchini Congo. Tume maalum kuhusu Rwanda na Congo itakutana mjini Luanda July 12.”

Ofisi ya rais wa Angola imetoa taarifa inayofanana na iliyotolewa na ofisi ya rais wa Congo. Hakuna taarifa imetolewa na utawala wa Rwanda hadi wakati tunaandaa ripoti hii na maafisa wa Rwanda hawakupatikana.

M23 wamedhibithi sehemu 14 zaidi

Waasi wa M23 walidhibithi mji muhimu wa Bunagana.

Msemaji wa kundi la M23 maj. Willy Ngoma amesema kwamba waasi hao wamedhibithi sehemu zingine 14 kufikia sasa.

“Tumewashinda nguvu waasi wa FDLR, wanajeshi wa FARDC na wapiganaji wa Mai Mai na kudhibthi miji mingine kadhaa.”

Kulingana na taarifa ya Maj. Ngoma, miongoni mwa sehemu ambazo sasa zipo chini ya waasi wa M23 ni Pamoja na Bikenke, Kavumu, Bugina, Mbuzi, Kinihira, Matovu, Muhimbira, Shangi, Nkokwe, Nyabikona, Tanda, Rutsiro, Kashali na Bukima.

M23 wanasemaje kuhusu mkutano wa Angola?

Haijabainika iwapo waasi hao wataondoka sehemu hizo namna marais wa DRC, Angola na Rwanda wamekubaliana, ikitiliwa mkazo kwamba Rwanda imekataa kabisa kwamba haihusiki na mgogoro unaondelea mashariki mwa DRC.

Msemaji wa M23 Maj. Willy Ngoma, amesema kwamba “hatuna shida na mkutano huo. Tunaunga mkono bora tu wanayozungumzia na kukubaliana yazingatie matajwa yetu.”

DRC imedaikwamba Rwanda inataka kuiba madini yake, zimetishiana vita

Tshisekedi anashutumu Rwanda kwa kutaka kunufaika na utajiri mkubwa wa madini ya Congo ikiwemo dhahabu, Coltan yanayotumika kutengeneza vifaa vya elektroniki.

Tshisekedi amesema kwamba “uwezekano wa vita kutokea ni mkubwa. Iwapo uchokozi wa Rwanda unaendelea, hatutakaa tu. Sio kwamba hatuna nguvu.”

Naye Kagame akasema “Naitakia Congo mema lakini mabaya yakija, yatanipata kama nipo tayari.”

Serikali ya Congo imekubali pendekezo la jumuiya ya Afrika mashariki kutuma jeshi la Pamoja mashariki mwa Congo kupambana na makundi ya waasi yaliyo katika sehemu hiyo.

Maelfu ya raia wamekimbia sehemu hiyo, wengi wao wakiingia katika nchi Jirani ya Uganda kama wakimbizi.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG