Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 06:54

Kipchoge ashindwa kutetea taji lake London


Eliud Kipchoge (fulana nyeupe) katika moja ya mashindano yake
Eliud Kipchoge (fulana nyeupe) katika moja ya mashindano yake

Shura Kitata wa Ethiopia achukua ushindi wa mbio hizo za London katika sekunde za mwisho dhidi ya Mkenya Vincent Kepchumba

Eliud Kipchoge bingwa wa mbio za marathon alishindwa kutetea taji lake la London marathon Jumapili baada ya kuishiwa nguvu katika kilomita 35 za mbio hizo na kujikuta akimaliza katika nafasi ya nane.

Shura Kitata wa Ethiopia alichukua ushindi kwa kumtoka Vincent Kipchumba katika sekunde za mwisho kabisa na kumaliza mbio hizo katika muda wa saa 2, dakika 5 na sekunde 41. Kepchumba alimaliza wa pili sekunde moja baadaye na nafasi ya tatu ilichukuliwa na mkimbiaji mwingine kutoka Ethiopia Sisay Lemma katika muda wa saa 2, dakika 5 na sekunde 45.

Mwanadada Brigid Kosgei wa Kenya alifanikiwa kutetea taji lake la mbio hizo kwa upande wa wanawake akishinda katika muda wa saa 2, dakika 18 na sekunde 58. Kosgei mwenye umri wa miaka 26 sasa ameshinda mashindano ya Chicago na London marathon mara mbili mfululizo.

Brigid Kosgei akikata utepe kushinda mbio za London marathon
Brigid Kosgei akikata utepe kushinda mbio za London marathon

Sara Hall wa Marekani alichukua nafasi ya pili kwa upande wa wanawake katika muda wa saa 2, dakika 22 na sekunde moja.

Mbio za London marathon zilielekea kuwa kali mwaka huu zikiwapapambisha Eliud Kipchoge na Kenenisa Bekele wa Ethiopia ambao walidhaniwa kuwa na nafasi kubwa sana katika mbio hizo. Lakini hali ilianza kubadilika siku mbili kabla ya mbio pale Bekele alipotangaza kujitoa katika mbio hizo kutokana na maumivu aliyokuwa nayo.

Kujitoa kwa Bekele kuliwacha uwanja wazi kwa Kipchoge na ilielekea hivyo kwa sehemu kubwa ya mbio hizo ambazo mwaka huu hazikutumia njia ya kawaida badala yake ilikuwa mizunguko ya eneo maalum lililotengwa.

Lakini hali ilianza kubadilika katika kilomita ya 35 pale Kipchoge alipoanza kupunguza kasi na kundi la akina Kitata, Kepchumba, Lemma na wengine wakachukua fursa hiyo kumtoka haraka bingwa huyo wa dunia.

XS
SM
MD
LG