Mashahidi magharibi mwa Libya wamesema waasi wamechukua udhibiti wa mpaka unaokatisha Tunisia kufuatia mapigano makali na vikosi vya usalama vinavyounga mkono serikali.
Shirika la habari la serikali la Libya limesema wanajeshi 13 wakiwemo kanali mmoja kamanda wamekatisha mpaka kuingia Tunisia kufuatia ghasia kali na majeshi yanayounga mkono serikali.
Vyombo kadhaa vya habari vimenukuu mashahidi wakisema kuwa waliona wanajeshi zaidi ya 100 wakijisalimisha kwa kukimbilia Tunisia.
Taarifa zinasema waasi walichukua eneo hilo upande wa mpaka wa Libya katika barabara inayoelekea kwenye mji wa Tunisia wa Dehiba. Majeshi yanayomuunga mkono kiongozi wa Libya moammar gadhafi yalikimbilia kukatisha mpaka kuingia Tunisia kuepuka kukamatwa na waasi.
Vyombo vya habari vya Libya vimeripoti kwamba majeshi ya NATO yalivamia jana jioni nje ya mji mkuu, Tripoli na kuuwa watu saba na kujeruhi wengine 18.