Timu ya Los Angeles Lakers imerudi katika kilele cha mpira wa kikapu Marekani kwa kushinda ligi ya NBA msimu huu baada ya kuishinda Miami Heat 106-93 katika mechi ya sita ya fainali za ligi hiyo. Lakers imeshinda mechi 4-2.
Ni mara ya 17 kwa LA Lakers kuchukua ubingwa wa NBA ikiwa sasa inafungana na timu ya Boston Celtics katika historia ya ligi hiyo.
Mara ya mwisho Lakers kufika fainali za NBA ilikuwa mwaka 2010, marehemu Kobe Bryant aliposhinda ubingwa wake wa tano. Bryant na binti yake Gianna na watu wengine saba, walifariki katika ajali ya helikopta January 26.
Huu ni ubingwa wa nne kwa LeBron James, ambaye amecheza katika fainali yake ya 10. James ameshinda ubingwa wa NBA na timu za Miami Heat (2012 na 2013), na Cleveland Cavaliers (2016). James alimaliza mechi ya Jumapili akiwa na pointi 28 na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa fainali za NBA kwa mara ya nne.
Msimu huu wa NBA ulikuwa mrefu kuliko yote baada ya ligi kusimamishwa mwezi March kutokana na janga la corona. Baadaye mechi za NBA zilihamishiwa katika uwanja maalum katika mji wa Orlando, Florida ambako timu 22 zilizokuwa zikiongoza ligi zilialikwa kucheza mechi zao zote katika ukumbi wa Walt Disney World Resort.