Kushner ambaye ni mkwe wa Rais wa Marekani Donald Trump na mshauri wake wa ngazi ya juu aliomba mawasiliano hayo ya siri yawe kati ya timu ya mpito ya Trump na ikulu ya Kremlin.
Gazeti hilo limemnukuu afisa wa Marekani Ijumaa akisema kuwa kitendo hicho kilikusudia kulinda mazungumzo yao kabla ya kuapishwa rais ili yasichungunzwe.
Vyanzo vya habari vya gazeti hilo vimesema balozi Sergei Kislyak ameripoti kwa wakubwa wake Moscow kuwa Kushner alitoa pendekezo hilo wakati wa mkutano wao mapema Disemba wakiwa katika Jumba la Ghorofa la Trump huko New York City.
Vyanzo hivyo vimesema taarifa hiyo ilinaswa kupitia mazungumzo ya Russia ambayo yalipitiwa na maafisa wa Marekani.
Siku ya Alhamisi, vyombo vya habari viliripoti kuwa Kushner anachunguzwa na FBI katika utafiti wao kuwa inawezekana kuwa kulikuwa na ushirikiano (wa udukuzi) kati ya kampeni ya Trump na Russia.
Gazeti hilo limeripoti pia wiki iliyopita kwamba afisa wa ngazi ya juu wa White House ambaye yuko karibu na rais alikuwa ndiye mlengwa muhimu katika uchunguzi huu uliokuwa nyeti, japokuwa haukutaja kwamba mtu huyo ni Kushner katika kipindi hicho.
Uchunguzi wa FBI hivi sasa unavyomfuatilia Kushner haimanishi kwamba lazima ni mshukiwa wa jinai, na wala hachukuliwi kuwa ndiye mlengwa wa uchunguzi mpana zaidi wa FBI dhidi ya Russia.