Wagambia walijitokeza kwa wingi mkubwa Jumamosi, kulingana na maafisa wa uchaguzi, ili kushiriki kwenye uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia katika muda wa miaka 27 bila ya kuwepo kwa jina la kiongozi wa zamani wa kimabavu Yahya Jammeh.
Uchaguzi huu unafuatiliwa kwa karibu kabisa kwani ni mtihani kwa demokrasia changa ya taifa hilo dogo la Afrika Magharibi.
Upigaji kura nchini humo ni wa kipekee ambapo kila mgombea ana kua na sanduku lake la kura na wapiga kura wanatumbukiza gololi iliyotengenezwa maalum kwa ajili ya uchaguzi.
Hii ni kutokana na hali kwamba watu wengi kati ya wakazi milioni 2 wa Gambia hawajui kusoma wale kuandika na hivyo hakuna vyeti vya kupiga kura.
Kiongozi wa kimabavu Jammeh alilazimika kukimbia uhamishoni Equatorial Guinea Januari baada kukataa kushindwa na Adama Barrow hapo Januari 2017.
Ingawa hakuweza kushiriki kwenye uchaguzi huo lakini inaripotiwa amekua na ushawishi mkubwa miongoni mwa wafuasi wake.
Rais Barrow mwenye umri wa miaka 56 anagombania kwa mhula wa pili akikabiliwa na upinzani kutoka wagombea watano akiwemo waziri wake wa zamani wa mambo ya kigeni anaeongoza upande wa upinzani, mwanasiasa mkongwe Ousainou Darboe.
Wagambia ambao kulingana na Benki Kuu ya dunia ndio watu maskini duniani wanataka mabadiliko ya kweli na ya dhati ya kiuchumi. Wengi walompigia kura Barrow kwenye uchaguzi wa 2016 wanasema hawajaridhika na uwongozi wake kwani hajaleta mabadiliko ya kubadili maisha yao.
Vyanzo vya habari hii ni AFP.