Kitengo cha habari cha kundi la Jama’ at Nursat al-Islam wal Muslimeen (NIM), kimesema katika taarifa kwamba wapiganaji wa kundi hilo walipambana na mamluki hao Jumamosi katika jimbo la Mopti, kulingana na tafsiri ya tovuti ya kundi la ujasusi, ambalo linafuatia taarifa za kundi hilo la wanamgambo wa kiislamu.
Wagner haina mwakilishi wa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari na haikuweza kupatikana ili kutoa maelezo.
Mali inatatizika kukomesha uasi wa wanamgambo wa Kiislamu uliokita mizizi baada ya ghasia za 2012 na kuenea tangu wakati huo katika nchi jirani, na kuua maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuhama makazi yao katika eneo la Sahel la Afrika magharibi.
Wagner ilianza kupeleka mamia ya wapiganaji mwaka jana kuunga mkono jeshi la Mali na imeshtumiwa tangu wakati huo na makundi ya haki za binadamu na wakazi kwa kushiriki katika mauaji ya raia, na kundi hilo halijatoa maelezo juu ya tuhuma hizo.
Serikali ya Russia ilikiri kwamba kuna wafanyakazi wa Wagner ambao wako nchini Mali lakini serikali ya Mali iliwaelezea kama wakufunzi kutoka jeshi la Russia badala ya makandarasi wa usalama wa kibinafsi.