O’Reilly alimwita Putin “muuaji” baada ya Trump kusema kuwa anamheshimu kiongozi huyo wa Russia.
“Maneno kama haya kutoka kwa mwandishi wa Fox News hayakubaliki na ni matusi, na kwa kusema kweli, tunapendelea tuombwe radhi na kituo hicho ambacho tunakiheshimu,” msemaji wa Putin, Dmitry Peskov amesema Jumatatu katika mkutano na waandishi wa habari.
Wakati O’Reilly alipomuuliza rais kuhusu kile mwandishi alichokiita “mauaji” yaliofanywa na Putin katika siku za nyuma, na vipi Trump angeweza kumheshimu pamoja na kujua historia hii, Trump amesema “Kuna wauaji wengi. Sisi pia tuna wauaji wengi. Unafikiria nini? Kwamba nchi yetu haina hatia?”
Maoni ya Trump yamewaudhi baadhi ya wanachama wa chama cha rais cha Republikan. Kiongozi wa walio wengi katika Baraza la Seneti Mitch McConnell amesema hafikirii tunaweza “kuilinganisha” Marekani na Putin. McConnell alimuelezea Putin, jasusi wa zamani wa KGB, kama “mhuni mmoja.”
Mashirika ya kipelelezi ya Marekani yameishutumu Russia kwa udukuzi uliofanywa kwenye kompyuta za chama cha Demokratik ikiwa ni sehemu ya kampeni pana iliyolenga kuvuruga uchaguzi wa urais wa Marekani.
Kabla ya kuchukua madaraka, Trump alirejea kudadisi taarifa za jumuiya ya kipelelezi. Lakini kukosoa huko kumesita kwa muda sasa. Lakini bado rais ameendelea kusema hadharani yuko tayari kuwa na mahusiano mazuri na Russia.
Trump na Putin walizungumza kwa simu hivi karibuni kile White House ilichokielezea kama “mwanzo mzuri wa kuboresha mahusiano kati ya Marekani na Russia uliokuwa unahitaji hatua hiyo.”
Mahojiano ya Fox News yamezungumzia swali linalosema Trump aliitisha uchunguzi juu ya wizi wa kura katika uchaguzi wa rais wa Novemba. Trump ametoa madai mengi kwamba wahamiaji haramu waliopiga kura wamesababisha yeye kukosa kura za umaarufu. Trump alishinda kura za wajumbe “Electoral College” na kumshinda mpinzani wake Mdemokrat Hillary Clinton, lakini alipoteza kura za umaarufu karibuni milioni tatu.
“Niacheni niwaambie mnapoona wahamiaji haramu—watu ambao sio raia na wako katika orodha iliyosajiliwa kupiga kura,” Trump alisema. “Kuna wahamiaji haramu, kuna watu waliokwisha kufa. Ni hali mbaya kwa kweli, ni mbaya kweli kweli.”
Maafisa wa uchaguzi waliochambua kura za Novemba 8 wanasema kuwa hakukuwa na dalili yoyote ya wizi wa kura, bila shaka sio kwa kiwango ambacho Trump anaelezea.