Baada ya mkutano wao huko White House, Gonzalez alisema kuwa alikuwa na mazunguzo marefu yaliyokuwa na tija na ya kirafiki, na Biden. “Kwa hakika tuliishukuru serikali ya Marekani kwa uungaji mkono wake kwenye vita vya kurejesha demokrasia ya Venezuela.” Gonzalez pia alisema alikuwa na matarajio kwa uhusiano wa karibu na utawala mpya wa rais mteule Donald Trump.
Mkutano kati ya Gonzalez na Biden ulifanyika siku chache kabla ya Maduro kuapishwa kuwa rais kwa muhula wa tatu Ijumaa. Maduro ameendelea kushikilia kuwa alishinda kwenye uchaguzi wa Julai, licha ya kwamba tume ya uchaguzi haikutoa hesabu ya kura kufuatia zoezi hilo. Upinzani kwa upande wake unashikilia kuwa hesabu zake kutoka kwenye zaidi ya asilimia 80 ya vituo zinaonyesha wazi kuwa Gonzalez alishinda uchaguzi huo kwa kura nyingi.
Marekani, mataifa mengi ya Ulaya pamoja na kadhaa ya Latin Amerika yamekataa kutambua ushindi wa Maduro, ambao umetambuliwa na mahakama ya Juu ya Venezuela pamoja na tume ya uchaguzi. Uchaguzi huo wenye utata ulizua maandamano makubwa yaliyopelekea vifo vya karibu watu 30, huku wengine zaidi ya 2,400 wakikamatwa.
Gonzalez ambaye ni mwanadiplomasia wa muda mrefu mwenye umri wa miaka 75, tangu uchaguzi huo amekuwa akiishi uhamishoni nchini Uhispania, wakati akiahidi kurejea Venezuela ili kuapishwa kuwa rais Ijumaa.
Forum