Kimbunga Mocha kilitua Jumapili alasiri katika jimbo la Rakhine la Myanmar karibu na kitongoji cha Sittwe kikiambatana na upepo wa hadi kilomita 209 kwa saa, idara ya hali ya hewa ya Myanmar ilisema.
Dhoruba hiyo awali ilipita kwenye kisiwa cha Saint Martins cha Bangladesh, na kusababisha uharibifu na majeruhi, lakini kiligeuka kutoka pwani ya nchi kabla ya kugeuza mwelekeo.
Usiku ulipoingia, ukubwa wa uharibifu huko Sittwe haukuwa wazi.
Mapema siku hiyo, upepo mkali ulibomoa minara ya simu, na kukata mawasiliano katika sehemu kubwa ya eneo hilo. Katika video zilizokusanywa na vyombo vya habari kabla ya mawasiliano kukatika, maji mengi yalipita barabarani huku upepo ukipiga miti na kung'oa mbao kwenye paa za nyumba.