Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Novemba 25, 2024 Local time: 05:11

Kikwete aiambia AU "wakati wa maneno matupu umekwisha"


Rais wa zamani wa Tanzania akizungumza wakati wa mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa,Ethiopia. Jumatano Januari 24, 2018. Picha| BMJ Muriithi, VOA.
Rais wa zamani wa Tanzania akizungumza wakati wa mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa,Ethiopia. Jumatano Januari 24, 2018. Picha| BMJ Muriithi, VOA.

Aliyekuwa rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Jumatano aliuambia mkutano mkuu wa Umoja wa Afrika kwamba wakati wa maneno matupu kuhusu kuwashirikisha wasichana katika masomo ya Teknolojia na sayansi umekwisha, na kwamba ni wajibu wa serikali za nchi wanachama kufadhili programu za elimu maarufu 'STEM' na kuwaangazia wasichana, sambamba na mapendekezo ya tume ya Umoja huo.

Akizungumza wakati wa mkutano wa 30 wa Umoja huo mjini Addis Ababa, Ethiopia, Kikwete, ambaye ni mwanachama wa tume ya kimataifa kuhusu ufadhili wa elimu duniani, alisema kuwa takwimu kuhusu masomo ya Sayansi barani Afrika bado zinaonyesha watoto wa kike wamesalia nyuma mno.

Alisema wakati wa mazungumzo na hotuba umekwisha.

"Ni lazima nchi binafsi zionyeshe uwajibikaji na wala siyo mazungumzo tu," alisema Kikwete.

"Ni wakati wa nchi wanachama wa AU kuchukua hatua madhubuti ambazo zitalipatia suala hili msingi imara wa kisheria na kitaasisi."

Kikao cha Jumatano kiliongozwa na kituo cha kimataifa cha Umoja wa Afrika kinachoshughulika na masuala ya wanawake na wasichana (AU/CIEFFA) na ubalozi wa Norway nchini Ethiopia.

Kilihudhuriwa pia na waziri wa mambo ya nje wa Norway, Ine Eriksen Soereide na mawaziri kadhaa wa elimu kutoka nchi wanachama wa AU.

Jumatatu, mabalozi wa nchi 55 wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ambao wanawakilisha nchi zao kwenye makao makuu mjini Adis Ababa walihudhuria kikao cha kuratibu masuala muhimu yatakayojadiliwa wakati wa mkutano huo utakaoendelea hadi tarehe 30 mwezi huu.

Baada ya kufunguliwa rasmi kwa mkutano huo, mabalozi hao waliendelea na kikao chao ambacho kitafuatiwa na kile cha baraza kuu la Umoja huo, kitakachohudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa AU.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni "kupambana na ufisadi." Moussa Faki Mahamat alisema kuwa tume ya Umoja wa Afrika inalipa umuhimu mkubwa suala hilo hususan kwa sababu ya hali mbaya inayoendelea kuripotiwa ya kukithiri kwa "janga" hilo katika mataifa mengi ya bara hilo.

Wakati wa ufunguzi huo, Mwenyekiti huyo alisema ni wakati muafaka kwa taasisi zote za Umoja wa Afrika kutafakari yale yaliyoweza kutekelezwa na yale ambayo hayajatimizwa na tume hiyo, katika kipindi cha miezi sita tangu mkutano wa mwisho ulipofanyika mwaka jana.

Mahamat alisema moja ya makubaliano muhimu yanayotarajiwa wakati wa kikao cha mwaka huu ni kuhusu azimio la kuwa na hati ya kusafiria kwa raia wa bara la Afrika kutoka nchi moja ya Afrika hadi nyingine bila pingamizi.

"Hii ni hatua ambayo wakati wake umefika. Hatimaye Waafrika wataacha kuwa wageni kwenye bara lao huku wageni kutoka nchi za nje wakitembea bila vizingiti vyovyote," alisema Mahamat.

Alisema kuwa kongamano la mwaka huu pia litashuhudia uzinduzi wa mradi wa usafiri wa anga wa pamoja katika bara la Afrika kufuatia azimio la mwaka 1999 la Yamoussoukro, Ivory Coast.

Tayari nchi 23 zimetia saini makubaliano hayo zikiwemo Kenya na Rwanda katika kanda ya Afrika Mashariki.

Masuala mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na njia mpya za kuimarisha kilimo barani Afrika, Sayansi na Teknolojia, uongozi bora na kadhalika.

Mkutano huo pia utajadili pendekezo la mwaka wa 2017 kuhusu haja ya kufanya mabadiliko makubwa ya kitaasisi kwa umoja huo.

Mkutano huo unafanyika wiki moja baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuripotiwa kutumia maneno ya matusi yaliyolenga nchi za bara la Afrika na Haiti, na kupelekea Umoja wa Afrika kutuma ujumbe kwa Trump, ukimtaka aombe msamaha.

XS
SM
MD
LG