Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 20:12

Kikao cha kila mwaka cha UN kuhusu haki za binadamu chaanza Geneva, Uswizi


Kamishna mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu Michelle Bachelet
Kamishna mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu Michelle Bachelet

Baraza la Umoja wa mataifa la haki za binadamu lilianza kikao chake cha kila mwaka Jumatatu mjini Geneva, na katika hotuba yake ya ufunguzi, Kamishna mkuu wa baraza hilo Michele Bachelet ameonya kwamba mabadiliko ya hali ya hewa na uchafuzi wa mazingira, ni tishio kubwa kwa haki za binadamu na ubinadamu wenyewe.

Mkuu huyo wa baraza la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu anasema binadamu kushindwa kuchukua hatua wakati kuna majanga ya sayari, imesababisha athari kubwa kwa haki nyingi, ikiwemo haki ya chakula cha kutosha, maji, elimu, afya, na hata maisha yenyewe.

Michele Bachelet anasema matukio makali na mabaya ya hali ya hewa yamewakumba watu katika kila eneo katika miezi ya hivi karibuni.

“Mioto mikubwa huko Siberia na California, mafuriko ya gafla huko China, Ujerumani na Uturuki, joto kali la eneo la Arctic ambalo limesababisha gesi chafu ya methane, na kuendelea kwa ukame usiokwisha kutoka Morocco na Senegal hadi Siberia, umewaweka ma millioni ya watu katika umaskini, njaa na kuwakosesha makazi yao,” alisema.

Bachelet ameonya kwamba tishio la mazingira linaloongezeka ni changamoto moja kubwa kwa haki za binadamu. Anasema majanga ya mazingira huongeza mizozo, mivutano, huongeza udhaifu na ukosefu wa muundo wa usawa kote ulimwenguni.

Kwa mfano, anabaini kuwa dharura ya kibinadamu katika nchi za Afrika eneo la Sahel imechochewa na mabadiliko ya hali ya hewa. Anasema ukame wa muda mrefu unaofuatiwa na mafuriko, ukosefu wa usawa kwa kupata rasilimali, viwango vya juu ya ukosefu wa ajira vinalisibu eneo hilo.

“Matatizo haya yanalazimisha watu kuhama makazi yao, yanazidisha mizozo na machafuko ya kisiasa, yanachochea makundi yenye itikadi kali kuajiri wapiganaji. Katika hali kama hiyo, lazima ielezwe wazi kwamba hakuwezi kuwa suluhisho la kijeshi kwenye mizozo katika eneo hilo. Kufikia sasa, watu milioni nne eneo lote la Sahel wamehama makazi yao, kulingana na makadirio ya UNHCR,” aliongeza.

Bachelet anasema matatizo na changamoto kama hizo zipo katika aina tofauti na kwa viwango tofauti katika maeneo yote ya ulimwengu.

Kwa mfano, Asia, mashariki ya kati na Afrika kaskazini, yamekumbwa na uhaba wa maji na kusabisha mivutano kuongezeka juu ya rasilimali hii nadra.

Anaripoti kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yana athari mbaya kwenye umaskini, watu waliohama makazi yao, na haki msingi za binadamu huko Guatemala, El Salvador na Honduras.

Anasema watetezi wa mazingira na haki za binadamu wanafanyiwa vitisho, wananyanyaswa, na hata kuuawa, mara nyingi wahusika hawaadhibiwi kabisa huko Amerika Kusini, kusini mashariki mwa Asia na maeneo mengine.

Mkuu huyo wa baraza la Umoja wa mataifa la haki za binadamu anasema mazingira salama, safi, yenye afya na endelevu, ndio msingi wa maisha ya mwanadamu.

Anaongeza kuwa mstakabali wa binadamu unategemea serikali zinazowajibika ili kuhifadhi rasilimali za ulimwengu.

-Ripoti imeandikwa na Lisa Schlein na kutafsiriwa na Patrick Nduwimana.

XS
SM
MD
LG