Kenyatta aliunda nafasi ya katibu mkuu wa utawala (Chief Administrative Secretary) kwenye wizara zote 22.
Wakati wa muhula wake wa kwanza, rais huyo alikuwa na mawaziri 18 kwenya baraza lake.
Hata hivyo, kufuatia uchaguzi wa mwaka jana, kumekuwa na shinikizo kumtaka aongeze idadi ya mawaziri, huku baadhi ya wakenya wakisema ni muhimu mno kwake "kutoa nafasi kwa jamii zote za Kenya ili kushiriki serikalini."
Kenyatta aliteua baraza lote la mawaziri takriban mwezi mmoja na nusu tangu kutangazwa mshindi wa urais na mahakama ya juu ya nchi hiyo.
Mapema mwezi huu, alitangaza mawaziri tisa, hatua ambayo ilikosolewa na baadhi ya Wakenya hususan kwa sababu hakutaja hata jina moja la mwanamke kwenye uteuzi huo.
Hata hivyo, orodha iliyotolewa Ijumaa ilikuwa na wanawake sita. Baadhi ya watu waliopoteza nafasi zao kwenye uchaguzi wa Agosti 8, 2017, waliteuliwa aidha kama mawaziri, makatibu wa wizara au mabalozi.
"Baada ya kushauriana na wadaiu mbalimbali, nimeamua kuwateua watu wafuatao kusaidia katika utekelezaji wa kazi za serikali," alisema Kenyatta katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja na vyombo ya habari nchini Kenya.
Mawaziri sita ambao walikuwa wanahudumu katika serikali yake muhula uliopita waliachishwa kazi hiyo na kuteuliwa kuwa mabalozi.
Baada ya Tanzania kukaa kwa muda mrefu bila mwanadiplomasia wa kiwango cha balozi wa Kenya kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa balozi wa Kenya nchini humo Chirau Ali Mwakwere hapo mwaka jana ili kuwania kiti cha ugavana katika uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, sasa Kenyatta amemteua Dan Kazungu, ambaye amekuwa waziri wa madini, kuchukua nafasi hiyo.
Amina Mohamed, ambaye alihudumu kama waziri wa mambo ya nje, amehamishiwa kwenye wizara ya elimu. Wizara ya mambo ya nje sasa imepewa aliyekuwa katibu wa wizara hiyo hiyo, Monica Juma.
Mbunge wa zamani Ababu Namwamba atakuwa baadhi ya watu wa kwanza kuchukua wadhifa mpya kabisa wa katibu mkuu wa utawala.
Haya yanajiri wakati muungano wa upinzani nchini humo (NASA), unashikilia kwamba rais Kenyatta hakuchaguliwa kihalali na kwamba wanachama wake hawamtambui kama rais.
Kiongozi wa muungano huo ameelezea nia yake ya kutaka kuapishwa kama "rais wa wananchi" tarehe 30 mwezi huu.
Balozi wa Kenya katika umoja wa mataifa, Macharia Kamau, ameteuliwa kama katibu wa kudumu katika wizara ya Afya, huku balozi wa Kenya nchini Uingereza Lazarus Amayo akiteuliwa kuchukua nafasi ya Kamau mjini New York.
Walioteuliwa watafika mbele ya kamati ya bunge ili kuidhinishwa au kukataliwa.
Hii ndiyo orodha kamili ya walioteuliwa:
- Waziri wa Fedha - Henry Rotich
- Waziri wa Afya - Sicily Kariuki
- Waziri wa Kawi - Charles Keter
- Waziri wa Utalii - Najib Balala
- Waziri wa Mambo ya Kigeni - Monica Juma
- Waziri wa Elimu - Amina Mohamed
- Waziri wa Kilimo - Mwangi Kiunjuri
- Waziri wa Viwanda - Aden Mohamed
- Waziri wa Ulinzi - Raychelle Omamo
- Waziri wa Usalama wa Ndani - Fred Matiang’i
- Waziri wa Michezo na Turathi - Rashid Mohamed
- Waziri wa Ugatuzi - Eugene Wamalwa
- Waziri wa Uchukuzi - James Macharia
- Waziri wa Teknolojia - Joe Mucheru
- Waziri wa Mazingira na Misitu - Keriako Tobiko
- Waziri wa Maji - Simon Chelugui
- Waziri wa Ardhi - Farida Karoney
- Waziri wa Mafuta na Madini - John Munyes
- Waziri wa E.A.C - Peter Munya.
- Waziri wa Utumishi kwa Umma,Vijana na Jinsia - Margaret Kobia
- Waziri bila kazi mahsusi - Raphael Tuju
- Waziri wa Leba - Ukur Yattani
MABALOZI:
Balozi wa Kenya nchini Ufaransa - Judy Wakhungu
Balozi wa Kenya Umoja wa Mataifa(Geneva) - Cleopas Mailu
Balozi wa Kenya nchini Tanzania - Dan Kazungu
Balozi wa Kenya, UNESCO (Paris) - Jacob Kaimenyi
Balozi wa Kenya, UN, New York - Lazarus Amayo
Balozi wa Kenya,Ubelgiji - Phylis Kandie
Balozi wa Kenya,India - Willy Bett
Balozi wa Kenya, Austria - Hassan Wario
Balozi wa Kenya, Uganda - Kiema Kilonzo
-Mwandishi wa Sauti ya Amerika, Kennedy Wandera amechangia ripoti hii.