Licha ya kwamba shule zote nchini Kenya zimefunguliwa, maafisa wa elimu wanasema kuwa siyo kila mwanafunzi, aliyefikia umri wa kwenda kwa shule ya upili, amefanikiwa kuingia darasani.
Mitandao ya kijamii nchini Kenya imejaa picha za wahitimu wa shule za msingi, wakiwa na mabango ya kuwaomba wahisani kuwasaidia karo ya shule ili waendelee na masomo.
Baadhi wamepokea msaada kutoka kwa wananchi wa kawaida na wafanyabiashara, na baadhi ya wanasiasa wamejitokeza kusaidia. hata hivyo, zaidi ya wiki mbili baada ya madarasa ya shule ya upili kuanza, takriban asili mia kumi ya wanafunzi milioni 1.3 ambao walifaulu mitihani ya kujiunga na shule za upili, mwaka jana, bado hawajafanikiwa kuingia darasani.
Serikali ya Kenya imekuwa ikishinikiza mpango wa asilimia 100 ya wanafunzi kutoka shule ya msingi hadi sekondari, lakini baadhi ya wanafunzi wanaona ugumu wa kuendelea na masomo kwa sababu za kifedha.
Lucy Njau ni mlezi wa Wambui, kijana aliyepata alama 354 kati ya 500 zinazohitajika. Njau anasema yeye ni maskini sana hawezi kumudu karo, sare na vitabu vinavyohitajika - shilingi 50,000, sawa na dola za Marekani 350 - kumpeleka Wambui shuleni.
"Ikiwa ninataka kumpeleka shuleni, nitatumia karibu shilingi 50,000, ikiwa ni pamoja na mahitaji yote ya shule na hata sare za shule ambazo siwezi kumudu," alisema
Kaunti za Laikipia, Nyeri, na Samburu zilirekodi kiwango asili mia 99 ya wanafunzi walioingia katika shule za sekondari, huku jiji kuu la Nairobi, pamoja na kaunti za Nakuru na Wajir zikirekodi asiloimia 98. Kaunti nyingine kadhaa zimeandikisha idadi ndogo kuliko hizo mbili.
Meshack Oduke ni mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari ya Shilce jijini Nairobi. Anasema wazazi wengi hawawezi kulipa ada zinazohitajika kuwaweka watoto wao darasani.
Anasema: "Sababu kubwa ni ada ya shule. Wazazi wengi wanashindwa kukusanya fedha zinazohitajika. Na ukiangalia ada za shule, za ziada za kaunti, ni takribanshilingi 50,000. Sasa kama wazazi hawa wanatoka kwa familia maskini, haitakuwa rahisi kwa mzazi kupata fedha zinazohitajika. Jambo lingine ni kwamba wapo wale wazazi ambao hawako tayari kuruhusu watoto wao, kuhamishwa kutoka eneo moja kwenda jingine, na hilo pia linaathiri mpango huo wa serikali."
Serikali ya Kenya hutoa msaada wa kifedha kwa wanafunzi wanaohitaji msaada, lakini sehemu kubwa zaidi inasalia kwa wazazi kulipa. Wakosoaji wanasema mfumo huo umejaa upendeleo na ufisadi, na kuwafungia nje wanaohitaji usaidizi zaidi.
Oduke anasema serikali inafaa kufikiria upya jinsi inavyotumia pesa za elimu kusaidia wanafunzi maskini.
"Serikali inafaa kuja na mpango ambapo fedha zote hizi zitawekwa kwenye kapu moja. Kisha, fedha hizi zipelekwe shuleni baada ya kuwabaini wanafunzi wenye uhitaji na wasio na uhitaji, kwa sababu tunaishia kufadhili au kutoa pesa hizi kwa wanafunzi ambao tayari wana uwezo wa kujilipia. Na wale ambao hawana uwezo wa kulipa, wanabaki nyumbani," anasema.
Maafisa wa Kenya wamezionya shule dhidi ya kuwafukuza wanafunzi kutokana na kukosa karo, lakini walimu wengi wanalalamikia ukosefu wa fedha za kuendesha shule kwa vile ni wanafunzi wachache wanaomaliza malipo yao kwa wakati.
Forum