Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 04:37

Kenya yapata kiti kwenye Baraza la Usalama la UN


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Kenya iliishinda Djibouti siku ya Alhamisi kufuatia duru ya pili ya uchaguzi uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani. Taifa hilo la Afrika Mashariki sasa litakuchukua nafasi isiyo ya kudumu kwenye baraza hilo kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia tarehe 1, Januari, mwakani.

Hayo yalijiri siku moja baada ya kutopatikana mshindi kati ya nchi hizo mbili, ambazo zilikuwa zimejitosa uwanjani kuwania nafasi hiyo.

Kenya hatimaye iliibuka mshindi baada ya kupata theluthi mbili ya kura zote zilizopigwa Alhamisi, kama inavyohitajika na kanuni za baraza hilo.

Nchi zipatazo 191 zilipiga kura, Kenya ikipata kura 129 huku Djibouti ikizoa kura 62.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alieleza fahari yake baada ya kufahamishwa kuhusu ushindi huo, akisema kwamba unaonyesha imani ambayo jumuiya ya kimataifa inayo kwa nchi yake.

Kenya ilitumia mbinu mbalimbali kujaribu kuzishawishi nchi zingine kuipigia kura. Ilimteua Tom Amolo kama balozi maalum wa kuiongoza kampeni hiyo, akisaidiwa na Balozi Catherine Mwangi na Lazarus Amayo, ambaye ni balozi wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Kenya kuketi kwenye baraza hilo. Ilikuwa moja ya wawakilishi wa bara la Afrika kati ya mwaka wa 1996 na 1997.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni chombo muhimu mno kwenye mfumo wa Umoja huo kwani lina nguvu za kufanya maamuzi yenye uzito mkubwa kimataifa.

Ingawa baraza hilo lina wanachama watano tu wa kudumu: Marekani, China, Russia, Ufaransa na Uingereza, ambazo kila mmoja ana kura ya turufu, nchi zingine kumi huwa zinawakilishwa kwa kipindi cha miaka miwili kila moja, na huwa zina ushawishi katika masuala mbalimbali.

Kwa sasa, Afrika inawakilishwa na Niger, Tunisia na Afrika Kusini kwenye baraza hilo. Hata hivyo, awamu ya Afrika Kusini inafika kikomo mwishoni mwa mwaka huu, na nafasi yake sasa itachukuliwa na Kenya.

Katika maeneo mengine duniani, Canada ilishindwa na Ireland na Norway kwenye uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali Jumatano, uliopekea Ireland kuomba usaidizi wa mwanamziki maarufu, Bono, na kupeleka wajumbe wa Umoja wa mataifa kwenye onyesho lake nchini Canada, na pia kupleeka wengine kwenye show ya mwanamuziki mwingine maarufu Celine Dion ili kuwarai kupiga kura.

Mexico na India zilichaguliwa bila kupingwa. Mataifa mapya kwenye baraza hilo lenye wajumbe 15 yataanza muhula wao wa miaka miwili Januari mosi mwaka 2021.

XS
SM
MD
LG