Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 08:49

Kenya yaadhimisha miaka 57 tangu kupata uhuru


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (Kulia) amkabidhi tuzo Mkenya mmoja ambaye hakutambulishwa wakati wa maadhimisho ya miaka 57 tangu nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa Uingereza.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (Kulia) amkabidhi tuzo Mkenya mmoja ambaye hakutambulishwa wakati wa maadhimisho ya miaka 57 tangu nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa Uingereza.

Kenya Jumamosi iliadhimisha miaka 57 tangu kupata uhuru kutoka kwa Uingereza. Hafla ya maadhimisho ya kitaifa ya siku maarufu kama 'Jamhuri Day,' iliongozwa na rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo katika uwanja wa Nyayo mjini Nairobi, Kenyatta alieleza hatua muhimu zilizochukuliwa na utawala wake tangu alipochukua hatamu za uongozi mnamo mwaka wa 2013.

Maadhimisho hayo yalijiri huku taifa hilo la Afrika Mashariki likikabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, ambayo, wachambuzi wanasema, kwa kiasi kikubwa, imesababishwa na janga la Corona.

Kwa mara nyingine, Kenyatta alitumia fursa hiyo kutetea msukumo unaoendelea wa kutaka kuifanyia marekebisho katiba ya Kenya, akieleza kwamba ndiyo njia ya pekee ya kupunguza uhasama unaojitokeza kila kipindi cha uchaguzi.

"Hali ya taharuki inayoshuhudiwa kila baada ya miaka mitano na ishara wazi kwamba katiba yetu ina mapungufu," alisema Rais Kenyatta.

Hata hivyo, aliongeza kwamba marekebisho hayo hayatatatua mizozo yote ya kikatiba nchini humo.

"Haya yatatakuwa marekebisho ya kwanza ya katiba ya 2010 na yanakusudiwa kuboresha katiba hiyo. Huu sio mwisho wa marekebisho kwani mengine yatafuata katika siku za usoni," alisema.

Azma ya kuifanyia marekebisho katiba ya Kenya imekuwa ikiibua hisia mseto, baadhi ya wananchi wakiipinga kwa misingi kwamba nia yake kubwa ni kuongeza nyadhifa za uongozi kwa wachache na kwamba huu si wakati muafaka kwa sababu ya mazingira ya janga la Corona.

Wakati wa maadhimisho ya Jumamosi, Kenyatta alitangaza kwamba serikali yake iko tayari kuhakikisha kwamba wanafunzi wote watarejea shuleni tarehe 4 mwezi Januari mwakani, baada ya kuwa likizoni kwa takriban miezi tisa kwa sababu ya cahangamoto za janga la Corona.

Baadhi ya wanafunzi tayari wamerejea shuleni na vyuoni.

Baadhi ya Wakenya walikuwa na hisia mseto kuhusu maadhimisho hayo.

John Kanyi Kinyua, aliandika kwenye mtandao wa Facebook: "Hizi hotuba tumezizoea. Hayo hayo ndiyo Kenyatta alisema mwaka jana. Ni nini kipya? Hakuna kitu kipya anatwambia isipokuwa mambo ya BBI ambayo yanakusudiwa kumpatia Kenyatta na mwanzake Raila Odinga nafasi kubwa za uongozi."

Mary Chebet naye alisema kupitia mtandao wa Twitter: "Naona Uhuru na Raila wana nia njema kwa Wakenya. Sidhani wanajitafutia tu madaraka. Hata hivyo, only time will tell (wakati tu ndio utaeleza).

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia na naibu wa rais William Ruto, Waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, Makamu wa rais wa zamani, Kalonzo Musyoka, na mke wa Rais Kenyatta, Margaret Kenyatta kati ya wengine.

Kenya ilipata uhuru wake kutoka Uingereza Tarehe 12 Desemba 1963, na bendera ya mkoloni, maarufu kama Union Jack, ikashushwa. Baada ya hapo bendera ya rangi nyeusi, nyekundu na kijani ikapandishwa kuashiria ujio wa taifa jipya.

Ilikadiriwa kwamba, mwaka wa 1963, Wazungu 55,800 waliishi nchini Kenya ambako idadi ya Waafrika ilikuwa takriban 8,366,000.

Wakenya walianza safari ya kutafuta uhuru mnamo miaka ya 1950, mbinu nyingi zikiongozwa na kundi la uasi la Mau Mau, vuguvugu la wanamgambo wa Kiafrika waliopingana na utawala wa kikoloni na unyonyaji wake dhidi ya wenyeji, hususan kuchukua ardhi yao kwa nguvu.

Wapiganaji wa vuguvugu hilo, ambao wengi wao walikuwa kutoka kabila kubwa la Kikuyu, waliwashambulia viongozi wa kikoloni na walowezi ambao nao walijibu kwa kuwakamata na kuwaua baadhi ya Wakenya hao.

Mwaka 1952, serikali ya kikoloni ikatangaza hali ya hatari na kuwakamata viongozi wengi wa kupigania uhuru nchini Kenya, akiwemo Jomo Kenyatta, babake rais wa sasa Uhuru Kenyatta, aliyekuwa rais wa chama cha Kenya African Union (KAA), ambacho baadaye kilibadilishwa jina na kuwa Kenya African National Union (KANU).

Kenyatta ambaye alikuwa waziri mkuu tangu mwaka wa 1963, aliapishwa kama rais wa kwanza wa nchi hiyo mnamo mwaka wa 1964.

XS
SM
MD
LG