Kenya imemaliza michezo ya Olimpiki ya Rio de Janeiro, Brazil ikiwa inaongoza bara la Afrika kwa medali. Kenya imeshinda jumla ya medali 13, ikiwa ni pamoja na sita za dhahabu, sita za fedha na moja ya shaba.
Kenya pia imeweka historia katika hiyo kwa kuwa nchi ya kwanza duniani kushinda mbio za marathon kwa wanawake na wanaume. Jemima Jelaget Sumgong alishinda marathon ya wanawake katika muda wa saa 2, dakika 24.04 wakati Eliud Kipchoge alifunga michezo ya Rio kwa ushindi wa marathon kwa wanaume katika muda wa saa 2, dakika 8.44.
Kenya ilifuatiwa na Afrika Kusini iliyoondoka na jumla ya medali 10, mbili zikiwa za dhahabu wakati Ethiopia ilishika nafasi ya tatu kwa Afrika ikiwa na jumla ya medali nane, moja ya dhahabu.
Miongoni mwa Wakenya walioshinda medali za dhahabu ni pamoja na bingwa wa dunia David Rudisha katika mita 800. Faith chepng'etich Kipyegon alishinda katika mita 1500 wakati Vivian Cheruiyot aliondoka na medali ya dhahabu katika mita 5000 na akafuatiwa katika nafasi ya pili na Hellen Onsando Obiri katika nafasi ya pili.
Naye Conseslus Kipruto alishinda medali ya dhahabu katika mita 3000 kuruka viunzi.
Mafanikio ya Kenya Rio yalikuwa sawa na yale ya michezo ya Olimpiki ya London mwaka 2012 ambapo ilimaliza na medali 12, lakini London iliondoka na medali mbili tu za dhahabu.