Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 19:58

Kenya ipo tayari kutuma wanajeshi wake DRC kupambana na waasi


Wanajeshi wa Kenya KDF katika mojawapo ya oparesheni ya kupambana na tukio la kigaidi jijini Nairobi Sept. 22, 2013.
Wanajeshi wa Kenya KDF katika mojawapo ya oparesheni ya kupambana na tukio la kigaidi jijini Nairobi Sept. 22, 2013.

Jeshi la Kenya KDF, linatayarisha kikosi chake kukituma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kama sehemu ya kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kupambana na makundi ya waasi ambayo yamepelekea kukosekana kwa amani sehemu hiyo.

Kikosi cha Kenya kimekabidhiwa bendera hii leo katika kambi ya jeshi ya Embakasi, Nairobi.

Kikosi cha Kenya kitakita kambi Kivu Kaskazini, ambapo kuna darzeni ya makundi ya waasi yanayoendelea kuwashambulia raia, kusababisha vifo, utekaji nyara na uharibifu wa mali.

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikubaliana hivi karibuni kutuma jeshi la pamoja kupambana na makundi ya waasi nchini DRC, ambayo yamekataa kuweka chini silaha.

Rais wa Kenya Dkt William Ruto ametangaza kwamba kikosi cha jeshi la Kenya kitaingia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo chini ya mpangilio wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupambana na makundi ya waasi.

Makundi ya waasi yameongeza mashambulizi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kuongeza uhasama wa kidiplomasia kati ya DRC na Rwanda.

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikubaliana mwezi Apriil kuunda kikosi cha jeshi la pamoja kuisaidia DRC kurejesha usalama na amani mashariki mwa nchi.

Akizungumza jijini Nairobi, Ruto amesema kwamba wanajeshi wa Kenya wanakwenda kufanya kazi ya kulinda binadamu.

"Kama majirani wenye ushirikiano mbalimbali, hali ya baadaye ya DRC inakaribiana na yetu. Sote tuna jukumu la kuisaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na usalama wake na tunajitolea kusaidia kurejesha utulivu nchini humo," amesema rais wa kenya William Ruto.

Rais Ruto ameongezea kwamba hawataruhusu makundi yenye silaha, wahalifu na magaidi kuwazuia kutekeleza wajibu wao.

Kenya itasimamia jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo pia litashirikisha wanajeshi kutoka Burundi, Uganda na Sudan Kusini.

Wanajeshi wa Rwanda watalinda usalama kwenye mpaka wa Rwanda na DRC baada ya Kinshasa kusema wanajeshi wa Rwanda wasishiriki katika operesheni hiyo ndani ya Congo.

Maafisa wa jeshi la Kenya hawajasema idadi ya wanajeshi wake wanaopelekewa DRC kwa sababu za kiusalama.

Wanajeshi wa Burundi na Uganda tayari wanapambana na waasi DRC

Jeshi la Burundi tayari limetuma kikosi chake nchini DRC, kupambanana na kundi la waasi la Red Tabara, sehemu za Kivu Kusini.

Jeshi la Uganda UPDF linapambana na waasi wa Allied Democratic Forces ADF, sehemu za Kivu Kaskazini.

DRC ilikataa kwamba haitaki wanajeshi wa Rwanda kuwa sehemu ya kikosi hicho kutokana na ukosefu wa imani na Rwanda, ambayo ilisema kwamba haijamshurutisha mtu yeyote kwamba ni lazima atume wanajeshi wake DRC.

Kenya inatuma kikosi chake wakati uhasama unaongezeka kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda.

Madai ya kuunga mkono makundi ya waasi wa M23

Waasi wa M23 wakiwa karuba, magharibi mwa mji wa Goma Nov. 28, 2022
Waasi wa M23 wakiwa karuba, magharibi mwa mji wa Goma Nov. 28, 2022

DRC inadai kwamba Rwanda inaunga mkono kundi la waasi la M23, madai ambayo Rwanda imekuwa ikiyakanusha kila mara, licha ya ripoti mbalimbali pia kudai hivyo.

Rwanda nayo inadai kwamba DRC inaliunga mkono kundi la waasi la FDLR ambalo linashutumiwa kusababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994. DRC imekana kabisa shutuma za kusiaidia FDLR.

Kundi la waasi la M23 limekataa kabisa kuondoka mji wa biashara wa Bunagana na limesema kwamba lipo tayari kwa vita.

Serikali ya DRC imesema kwamba haitafanya mazungumzo ya amani na kundi hilo, ambalo imelitaja kuwa ‘magaidi’.

Makubaliano ya jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki

Kulingana na mpango wa kijeshi uliokubaliwa na makamanda wa majeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sehemu za Ituri, Kivu Kaskazini (Bunagana, Bugusa, Petit Nord, Masisi, Lubero, Beni-Kamdini) na Kivu Kusini zitatangazwa kuwa sehemu ambazo silaha haramu hazikubaliwi na wanaozimiliki wanastahili kuzisalimisha kwa mamlaka.

Mtu yeyote au kundi lolote linalobeba silaha kinyume cha sheria litakabiliwa kwa nguvu za kijeshi.

Jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki litapiga kambi katika sehemu za Kivu Kaskazini na Kivu Kusini kuhakikisha kwamba kuna usalama. Jeshi la jumuiya litashirikiana na jeshi la Umoja wa Mataifa – MONUSCO.

XS
SM
MD
LG