Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 15, 2025 Local time: 15:03

Kenya katika hatari ya wimbi jipya la Corona


Waziri wa Afya, Kenya, Mutahi Kagwe
Waziri wa Afya, Kenya, Mutahi Kagwe

Kagwe anasema maafisa wa afya wanafuatilia mwenendo wa wanasiasa wanaokiuka maagizo ya kisayansi na kufanya mikutano ya kisiasa yenye mikusanyiko ya watu wengi.

Waziri wa Afya wa Kenya ameonya kwamba nchi hiyo ipo katika hatari kubwa ya kutokea wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya Corona, kwa sababu wanasiasa na vijana wanaendelea kukaidi maagizo ya maafisa wa afya, huku kiwango cha maambukizi kikiendelea kuongezeka.

Akihutubia waandishi wa habari, Jumapili, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, amesema kwamba kiwango cha maambukizi ya virusi vya Corona kimeongezeka nchini humo, akiripoti visa vipya 685 jumapili pekee.

Ameonya uwezekano wa “kutokea janga kubwa la kiafya” akieleza kwamba vijana wanaendelea “kupuuza hatari ya virusi hatari vya Corona.”

Waziri asikitika na kuonya hatari kubwa

Kagwe, amesema kwamba maafisa wa afya wanaendelea kufuatilia mwenendo wa wanasiasa wanaokiuka maagizo ya kisayansi na kufanya mikutano ya kisiasa yenye mikusanyiko ya watu, akionya kwamba huenda hatua kali zikalazimika kutumika kurejesha nidhamu kati ya raia.

Waziri huyo wa afya ameeleza masikitiko kwamba “watu walio omba sana shughuli za kawaida zifunguliwe, ndio wanaoongoza katika kukiuka maagizo ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona”.

“Hakuna shaka kwamba tunaelekea kushuhudia wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya Corona,” amesema Waziri Kagwe, akiongezea kwamba “iwapo viongozi hawatatilia maanani maagizo ya kiafya, wanapotosha raia kwamba kila kitu kipo sawa wakati hali ni mbaya. Lazima viongozi waajibike.”

"Hakuna ishara ya maambukizi kumalizika. Mtu akiambukizwa akiwa katika baa, anaweza kurudi nyumbani na kuwaambukiza watoto na maambukizi hayo kuendelea kusambaa kwa haraka. Tunaona hali ya watu kurejea katika maisha ya kawaida, hata maafisa wa afya wameanza kuzembea. Hatari ni kubwa” Ameonya Kagwe.

Kiwango cha maambukizi

Kulingana na Wizara ya Afya ya Kenya, kiwango cha maambukizi nchini humo kimefikia asilimia 12 kutoka asilimia 4 wakati serikali ilipolegeza masharti ya kupambana na virusi hivyo na kuruhusu raia kurejea hali yao ya maisha ilivyokuwa awali lakini kwa tahadhari.

Kufikia Jumapili tarehe 18 Oktoba, watu 28 wamelazwa katika chumba cha kuwahudumia wagonjwa mahtuti baada ya kuambukizwa virusi vya Corona, huku idadi ya jumla ya wagonjwa kutokana na virusi hivyo ikiwa imefikia watu 1,000.

Kaimu mkurugenzi wa huduma za afya nchini Kenya Patrick Amoth, amesema idadi ya wagongwa wanaolazwa hospitalini imeongezeka kutoka 450 hadi 991 katika mda wa siku moja. Wagonjwa 10 wanapumua kwa usaidizi wa machine, huku 14 wakiwa wameekewa oxygen.

Kati ya wagongwa ambao wamelazwa hospitalini, 50 ni raia wa kigeni.

Mji wa Nairobi unaongoza kwa maambukizi, ukifuatiwa na Nakuru, Mombasa, Trans Nzoia, Kisii, Kiambu, Kakamega, Kisumu, Busia, Kilisi na Nandi.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG