Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 08:41

Zaidi ya 200 wafariki katika ajali Kenya kabla Krismas


Moja ya ajali kubwa zilizotokea Kenya Disemba 2017
Moja ya ajali kubwa zilizotokea Kenya Disemba 2017

Serikali ya Kenya imetangaza tahadhari maalum za usalama barabarani wakati huu ambapo watu wanasafiri kwa ajili ya sikukuu za Krismas na mwaka mpya baada ya zaidi ya watu 200 kufariki katika ajali katika mwezi huu wa Disemba.

Hatua hiyo ya Kenya imefuatia ajali kadha mbaya ambazo zimetokea mwezi wa Disemba wakati ambapo watu wengi wanasafiri kwenda maeneo wanayotokea kusherehekea Krismas na mwaka mpya

Ikiwa imebaki chini ya wiki moja kabla ya sikukuu ya Krismas tahadhari inatolewa kwa waendesha magari, wasafiri na kampuni za usafirishaji kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuata ili kuepusha ajali.

Disemba 14 Idara ya usalama wa barabarani Kenya (NTSA) ilitoa taarifa iliyosema kuanzia Disemba mosi hadi 12 watu 150 walipoteza maisha katika ajali za barabani kote nchini Kenya. Idara hiyo ilisema nyingi ya ajali hizo zimesababishwa na makosa ya binadamu na zingeweza kuepukika.

Katika muda wa saa 24 Disemba 13 jumla ya watu zaidi ya 40 walifariki katika ajali za barabarani Kenya.

Jumapili Disemba 17 watu 17 walifariki katika ajali ya matatu na lori sehemu iitwayo Ngoliba katika barabara ya Thika-Garissa.

Jumapili hiyo hiyo watu watano walifariki kutokana na ajali iliyotokea Jumamosi katika eneo la Makutano kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret na kufanya jumla ya watu waliokufa katika ajali hiyo kufikia 10.

Ajali hiyo ya Makutano ilitokea katika eneo linajulikana la hatari kutokana na kupinda kwa barabara katika mlima wa Koibatek. Eneo hilo ni kilomita 15 kutoka sehemu ambapo wanamuziki 15 wa Kalenjin walifariki katika daraja la Kamara, kiasi cha kilomita 20 kutoka Sangangwan, sehemu nyingine mbaya ambapo watu kadha walifariki katika ajali iliyohusisha magari zaidi ya 13. Sehemu hiyo hatari ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 34 katika muda wa wiki moja.

NTSA inasema imeongeza doria za barabarani kuwakamata wale wanaovunja sheria za barabarani, kwenda kasi kupita kiasi na kusababisha ajali.

Idara hiyo pia imetaka madereva ambao magari yao yamepata hitilafu barabarani kuyaondoa na kuyaweka kando katika muda wa saa moja tu. Ajali kadha zimetokea kwa magari madogo kuingia katika mivungu ya malori ambayo yameharibika barabarani.

XS
SM
MD
LG