Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 08:04

Kamati ya Bunge ina wasiwasi na pendekezo la polisi Uganda


Jengo la Bunge la Uganda
Jengo la Bunge la Uganda

Jeshi la Polisi nchini Uganda limekabiliwa na upinzani mkubwa juu ya pendekezo lao la kuruhusu maafisa wao kuwashikilia washukiwa kwa kipindi cha zaidi ya siku mbili kabla ya watu hao kupewa dhamana au kufikishwa mahakamani.

Wakati polisi wakisema kuwa badiliko hilo litawaathiri wanaoshutumiwa kuwa magaidi, wanaopiga mabadiliko hayo wanasema wale waliotuhumiwa kwa uhalifu mdogo pia watazuiliwa na polisi kwa muda mrefu kupitia sheria hiyo.

Polisi wanasema kuwa aina fulani ya uhalifu, kama vile ugaidi, unahitaji uchunguzi ambao unafanyika nje ya mipaka ya nchi ili kukusanya ushahidi na mashahidi.

Serikali inajaribu kuomba waungwe mkono na bunge ili kubadilisha kifungu cha 23 cha Katiba ili polisi waweze kuwashikilia washukiwa wa ugaidi kwa kipindi cha siku saba hadi kumi na nne kabla ya kuwafikisha mahakamani.

Patrick Onyango ni naibu msemaji wa jeshi la polisi Uganda anasema: "Wakati mwengine tukiwa tunazichunguza hizi sampuli zilizochukuliwa kutoka katika eneo la uhalifu, pia muda unahitajika. Kwa sababu, sisi pia tunatumia maabara nyingine za serikali kuchunguza. Wao pia wanahitaji muda wa kufanya hilo. Wakati mwengine wanasema, sisi pia tumetingwa na kazi nyingi, pamoja na hizo sampuli mlizozileta. Hivyo basi tunawaomba wabunge katika baadhi ya kesi wanatakiwa kubadilisha katiba ili kuturuhusu kuwaweka washukiwa kwa angalau zaidi ya masaa 48.”

Kabla ya pendekezo hilo kuchukuliwa hatua, lazima liungwe mkono na Kamati ya Haki za Binadamu ya Bunge.

Jove Kamateka, ambaye ni mwenyekiti wa kamati, anasema ana mashaka juu ya hili. Anasema tayari polisi wanavunja sheria.

“Wameshindwa kuheshimu sheria katika kesi ndogo ndogo. Na tunafikiri kuwa hii sheria ilivyo hivi sasa, inawawezesha kuwapeleka washukiwa mahakamani, na kusema kuwa hauko tayari kuendelea na mashtaka. Na unaweza kuomba muda zaidi kuendelea na uchunguzi. La pili, rumande ya polisi haina nafasi ya kutosha kuwashikilia washutumiwa," amesema Kamateka.

Mwaka Jana, wakati polisi wakipeleleza mauaji ya Felix Kaweesi, naibu Inspekta jenerali wa polisi, washukiwa wa mauaji yake waliwekwa ndani kwa zaidi ya miezi mitano bila ya kufikishwa mahakamani.

Washukiwa wengine, wakiwemo watu wanaompinga Rais Yoweri Museveni, pia wamekuwa wanashikiliwa na polisi kwa zaidi ya masaa 48 kabla ya kufikishwa mahakamani au kupewa dhamana.

Tume ya Haki za Binadamu Uganda, taasisi ya serikali, imeendelea kukosoa polisi kwa kupuuzia kufuata sheria.

Mwenyekiti huyo wa tume hiyo, Meddie Mulumba anasema juhudi yoyote ya kuzuia ugaid ni lazima izingatie nguzo za msingi za haki za binadamu.

XS
SM
MD
LG