Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 15, 2025 Local time: 07:38

Kagame: Nipo tayari kuendelea kuongoza Rwanda kwa miaka 20 zaidi


Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul Kagame

Rais wa Rwanda Paul Kagame, amesema kwamba haoni shida yoyote akiendelea kuongoza Rwanda kwa miaka mingine 20, na kuashiria kwamba atagombea muhula mwingine madarakani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024.

Kagame, mwenye umri wa miaka 64, ametawala Rwanda kwa zaidi ya miongo miwili. Amesema kwamba anajiandaa kwa muhula mwingine madarakani.

Katika mahojiano na shirika la Habari la Ufaransa France 24, Ijumaa (Julai 8, 2022), Kagame amesema kwamba “nafikiria kuendelea kuongoza kwa miaka mingine 20. Sina shida na hilo. Uchaguzi unahusu watu kufanya maamuzi kuhusu wale wanaotaka wawe viongozi wao.”

Mabadiliko ya katiba

Kagame alishinda uchaguzi wa mwaka 2017 kwa asilimia 99 ya kura zilizopigwa baada ya kubadilisha katiba na kuondoa kikomo cha mihula miwili kwa wagombea urais.

Mabadiliko hayo yalimuongezea Kagame muda wa kutawala Rwanda kwa muhula mwingine wa miaka 7.

Muhula wake wa sasa wa miaka 7 utakapokamilika, Kagame atakuwa na haki kisheria kugombea tena mihula mingine miwili ya miaka 5, kulingana na mabadiliko ya katiba yaliyofanywa.

Hatua ya kubadilisha katiba, ilitoa fursa kwa Kagame kuanza upya utawala wake na kupata nafasi ya kutawala Rwanda hadi mwaka 2034.

Kagame alikuwa amesema kwamba hatagombea tena urais

Kagame alikuwa na umri wa miaka 36 alipoongoza chama chake cha Patriotic Front, na kuwaondoa madarakani viongozi wa Kihutu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya karibu watu 800,000 wengi wao wakiwa Watutsi kati ya mwezi Aprili na Julai mwaka 1994.

Utawala wake umetuhumiwa kwa ukandamizaji wa haki za kibinadamu na ukosefu wa uhuru wa kujieleza na demokrasia.

Wakosoaji wake wamekamatwa na kufungwa gerezani.

Amenadi sera zake kote ulimwenguni kama kiongozi mwenye maono makubwa ya maendeleo na kusifia ukuaji wa uchumi nchini mwake, japo wachambuzi wanasema hakuna uhuru wa aina yoyote ikiwemo vyombo vya Habari kueleza wazi kinachoendelea ndani ya Rwanda.

Mnamo mwezi Desemba mwaka 2019, Rais Kagame alisema kwamba hakuwa na nia ya kugombea tena urais ifikapo mwaka 2024.

Alikuwa akizungumza katika kongamano la viongozi mjini Doha Qatar, ambapo alisema kwamba alikuwa tayari kutoa fursa kwa watu wengine kuongoza Rwanda.

“Raia wa Rwanda ndio walitaka niendelee kuwa rais”

Mnamo mwaka 2017, Kagame alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba Rwanda inaweza kuongozwa vizuri sana na mtu mwingine hata kama hatakuwepo.

“Watu wa Rwanda walitaka niwe rais wao ndio maana walifanya mabadiliko ya katiba Desemba 2015 ili niendelee kufanya kazi nzuri ninayofanya. Nilikubali uamuzi wao. Lakini wakati umefika wanastahili kuanza kufikiria namna ya kuongoza nchi baada yangu,” alisema rais Paul Kagame mwaka 2017.

Mwaka 2012, Kagame aliliambia jarida la world Policy kwamba hatawahi kugombea mhula mwingine madarakani na kwamba alikuwa tayari kuheshimu katiba ya Rwanda namna ilivyokuwa, na kwamba angeondoka madarakani muda wake ukimalizika.

“Tuna katiba ambayo ina kikomo cha mihula kwa rais. Namalizia muhula wangu wa pili na wa mwisho. Nina matumaini kwamba mtu mwenye uwezo wa kuongoza Rwanda atakuwepo kuendelea na kazi ambayo nafanya bila kuirudhisha nyuma Rwanda ama kuharibu mipango iliyopo.”

Kagame aliwahi kuwa mwanajeshi wa ngazi ya juu Uganda

Paul Kagame alizaliwa mwezi Oktoba mwaka 1957, kusini mwa Rwanda. Familia yake ilikimbia mapigano ya kikabila mwaka 1960 na kuingia Uganda, ambapo aliishi kwa muda wa miaka 30 kama mkimbizi.

Aliungana na rais wa Uganda Yoweri Museveni na kuanzisha vita vilivyomwezesha Museveni kuingia madarakani, kabla ya Kagame kupewa cheo cha juu katika jeshi la Uganda chini ya utawala wa rais Museveni.

Alirudi nchini Rwanda mwaka 1990 na kuongoza chama cha Rwandan Patriotic Front RPF katika vita vya miaka 4 hadi Julai 1994.

Chama cha RPF kilianza juhudi za kuleta umoja na maridhiano, ujenzi wa taifa, maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Paul Kagame aliteuliwa kuwa naibu wa rais na waziri wa usalama katika serikali ya umoja wa kitaifa Julai 19,1994.

Alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama cha RPF miaka minne baadaye. RPF kilikuwa sehemu ya serikali ya umoja wa kitaifa.

April 22, 2000, alichukua uongozi kama rais wa Jamhuri ya Rwanda baada ya kuchaguliwa na baraza la mpito na kushinda uchaguzi mkuu wa kwanza wa kidemokrasia kuwahi kuandaliwa nchini Rwanda mnamo mwaka 2003.

Alichaguliwa kwa muhula wa pili wa miaka 7, mwaka 2010.

Uhusiano wa Rwanda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC.

Kagame ametangaza kuwa tayari kuendelea kuiongoza Rwanda wakati ambapo ametajwa sana katika vita vya waasi vinavyoendelea mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC.

DRC inamshutumu kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, japo amekana madai hayo mara kadhaa. Ametishia vita dhidi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo endapo itaendelea kufanya kile ambacho amekitaja kama uchokozi kwa kufyatua makombora ndani ya Rwanda.

“Naitakia Congo mema. Lakini mema yasipokuja, watanipata kama nimejitayarisha kwa mabaya zaidi. Najitayarisha kwa mabaya lakini nawatakia mema.Namaanisha ninachosema. Naitakia Congo mema, na naitakia mema nchi yangu ya Rwanda.” Alisema Kagame.

Ameishutumu DRC kwa kuwapa hifadhi waasi wa kundi la FDLR linalotuhumiwa kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

“Wapiganaji wa FDLR wamekuwa wakishirikiana na jeshi la Congo kupigana na kundi la M23, Umoja wa Mataifa nao ulijihusisha wakisema wanalisaidia jeshi la Congo lakini walijua jeshil a serikali lilikuwa linashirikiana na kundi la FDLR dhidi ya M23. Kundi la M23 lilikuwa linapambana na Monusco, jeshi la serikali na waasi wa FDLR. Kundi la FDLR lilistahili kuwa limepigwa, kumalizwa nguvu na kurudishwa nyumbani.” Amesema Kagame akiongezea kwamba “hayo ndio yamekuwa yakifanyika. wamekuwa wakirusha makombora ndani ya Rwanda, kuharibu mali na kusababisha vifo. Wamefanya hivyo mara kadhaa.”

Uhusiano wa Rwanda na majirani wake wengine

Rwanda vile vile ina uhusiano usio mzuri na jirani yake Uganda. Mpaka kati ya nchi hizo ulifungwa kwa muda mrefu, Rwanda ikidai kwamba Uganda ilikuwa inawakamata raia wake bila makosa yoyote, huku Uganda ikidai kwamba Kagame alikuwa anapanga kuupindua utawala wa rais Yoweri Museveni.

Uhusiano kati ya Rwanda na Burundi pia sio mzuri. Mnamo mwezi Mei mwaka huu, rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye alisema kwamba “uhusiano kati ya nchi hizo mbili utaanza kuimarika iwapo tu Rwanda itaikabidhi Burundi watu waliokuwa wamepanga kutekeleza mapinduzi ya mwaka 2015,” ambapo Burundi inaamini wanapewa hifadhi na serikali ya Paul Kagame.

Rwanda na Tanzania vile vile zilikuwa na uhusiano usiokuwa mzuri mwaka 2013 baada ya aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Kikwete kutoa ushauri kwamba ni vyema rais Paul Kagame afanye mazungumzo na waasi wa kundi la FDLR ili kumaliza uhasama kati yake na kundi hilo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG